Kuhuishwa uhusiano wa Hamas na Syria; kuimarisha muqawama katika eneo
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i88302-kuhuishwa_uhusiano_wa_hamas_na_syria_kuimarisha_muqawama_katika_eneo
Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) imetangaza kuwa inataka kuwa na uhusiano imara na Syria katika fremu ya uamuzi wake wa kuanzisha tena uhusiano na serikali ya Damascus.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Sep 18, 2022 06:47 UTC
  • Kuhuishwa uhusiano wa Hamas na Syria; kuimarisha muqawama katika eneo

Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) imetangaza kuwa inataka kuwa na uhusiano imara na Syria katika fremu ya uamuzi wake wa kuanzisha tena uhusiano na serikali ya Damascus.

Uhusiano wa Hamas na Syria ulikumbwa na mabadiliko tangu mwaka 2011. Hamas ilichukua uamuzi wa kufunga ofisi yake huko Damascus mji mkuu wa Syria kama radiamali yake kufuatia kuibuka mgogoro huko Syria ambapo uhusiano wa pande mbili ulikumbwa na hali ya mivutano. Hata hivyo baada ya kupita muongo mmoja, harakati ya Hamas ya Palestina kwa mara nyingine tena imeonyesha nia yake ya kutaka kuhuisha uhusiano na utawala wa Syria. Hamas imesema kuwa, kustawisha uhusiano huo ni sawa na kuwahudumia wananchi na kadhia ya Palestina; na kwamba suala hilo lina umuhimu mkubwa katika kivuli cha matukio yanayojiri kwa kasi ya kieneo na kimataifa yanayoizunguka Palestina. 

Syria pia siku zote imekuwa na mchango na nafasi muhimu katika kadhia ya Palestina kutokana na nafasi yake ya kijiografia na pia hatua yake ya kukabiliana moja kwa moja na utawala wa Kizayuni. Aidha Syria ni moja ya waungaji mkono wa jadi na wakuu wa muqawama wa Palestina mkabala wa utawala haramu wa Israel unaoikalia Quds Tukufu kwa mabavu. Pamoja na hayo, mwaka 2011 harakati hiyo ya mapambano ya Palestina ilikata uhusiano wake na serikali ya Damascus. Hamas ilichukua uamuzi huo huku mirengo ya kushoto na ya kizalendo ya makundi ya ndani ya kisiasa ya Palestina kama harakati ya Kidemokrasia ya Uhuru na  Harakati ya Ukombozi wa Palestina zikiendeleza uungaji mkono wao kwa serikali ya Damascus; na kutangaza kuwa mapinduzi ya Syria ni njama ya Uzayuni.  

Wanamuqawama wa Palestina 

Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) ilichukua uamuzi wa kutazama upya kimsingi uhusiano wake wa kisiasa na khususan na pande muhimu za muqawama katika eneo kufuatia kufanikiwa serikali ya Syria kudhibiti mgogoro wa ndani na kulinda umoja wa ardhi nzima ya nchi hiyo na vile vile mwaka 2017 baada ya Hamas kuendesha uchaguzi na kuchaguliwa Ismail Hania kuwa Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya harakati hiyo. Tokea wakati huo pia kumekuwa kukisikika tetesi za kuhuisha uhusiano wa Hamas na Syria na sasa hatua za kivitendo za utekelezaji zimechukuliwa katika uwanja huo. 

Kuhuishwa uhusiano wa pande mbili hizo kuna umuhimu kwa makundi ya muqawama. Katika mazingira ya hivi sasa ambapo baadhi ya nchi za Kiarabu zinafanya kila ziwezalo kuanzisha na kustawisha uhusiano wa kidiplomasia na utawala ghasibu wa Israel, kitendo cha  kuhuisha uhusiano na serikali ya Syria kinaweza kuyasaidia sana makundi ya mapambano ya Palestina ikiwemo harakati ya muqawama ya Hamas na pia kuimarisha nafasi ya muqawama wa Palestina katika eneo. Kuhusiana na hilo, Hani Al-Thawabitah mjumbe wa Kamati Kuu ya Harakati ya Wananchi kwa ajili ya Ukombozi wa Palestina amezungumzia kuhusu uamuzi wa harakati ya Hamas wa kurejesha uhusiano na serikali ya Syria kwamba, kustawisha uhusiano wa Waarabu na Palestina ni kwa maslahi ya kadhia ya Palestina. Amesisitiza kuwa, moja ya misingi ya nguvu ya kadhia ya Palestina ni kustawisha uhusiano kama huo na kwamba, kuanzishwa tena kwa uhusiano wa Hamas na Syria kutaimarisha mhimili wa muqawama katika eneo. 

Hani al Thawabitah 

Nukta muhimu hapa ni hi kuwa, Syria sawa na makundi mengine ya muqawama ya Palestina inatoa kipaumbele kwa suala la kukabiliana na utawala wa Kizayuni; ambapo utawala huo ni adui wa pamoja wa Hamas na Damascus. Kwa msingi huo, kuhuishwa uhusiano wa harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) na Damascus kutazidisha mshikamano wa mhimili wa muqawama mkabala wa utawala ghasibu wa Kizayuni. 

Khidhr Habib mmoja wa viongozi wa harakati ya Jihad Islami ya Palestina amekaribisha uamuzi wa Hamas wa kustawisha uhusiano na Syria na kusema: "Hii ni hatua iliyopigwa katika njia sahihi itakayopelekea kuboreshwa mhimili wa muqawama kwa ajili ya kukabiliana na adui Mzayuni. Syria ni nguzo muhimu katika mzozo na adui Mzayuni na misimamo yake ni imara na thabiti." Misimamo kama hii ni kwa maslahi ya kadhia ya Palestina, wananchi wake na Umma wa Kiarabu kwa ajili ya kukabiliana na mwenendo wa mapatano na utawala wa Kizayuni. 

Wakati huo huo Muhammad al Barim Mkuu wa Ofisi ya Vyombo vya Habari ya Kamati za muqawama wa Palestina ameeleza kuwa: Kuanzishwa tena uhusiano wa Hamas na Syria na kupanuliwa kwake kutaimarisha mhimili wa muqawama na kusimama imara mbele ya jinai za adui Mzayuni zinazoulenga Umma wa Kiarabu na Kiislamu.