Israel yafuta maeneo matakatifu ya Kiislamu katika ramani mpya
Wizara ya Utalii ya utawala wa Kizayuni wa Israel imechapisha ramani mpya ya mji wa Quds tukufu ambayo ndani yake maeneo yote matakatifu ya Kiislamu na Kikristo yamefutwa.
Ramani hiyo mpya inayosambazwa bila malipo na Wizara ya Utalii ya utawala huo haramu haina Masjidul Aqsa ambacho ni Kibla cha Kwanza cha Waislamu na wala al-Ḥaram al-Šarīf.
Aidha ramani hiyo mpya imefuta eneo lililo na Kanisa la Kikatoliki la Saint Anne ambalo liko karibu na eneo la Lions' Gate kama ambavyo imefuta pia Makanisa ya Flagellation and Condemnation, yaliyoko mashariki mwa Quds tukufu. Kadhalika Kanisa la Kilutheri la Redeemer, ambalo ni la pili kwa kuwa na wafuasi wengi kati ya Makanisa ya Kiprotestanti kwenye eneo la Quds, limeonyeshwa katika ramani hiyo kama kijisehemu kidogo ambacho ni vigumu kuonekana au kutambuliwa. Aziz Abu Sarah, mkaazi wa Quds tukufu amenukuliwa na shirika la habari la Tasnim akisema kuwa, ramani hiyo mpya inakusudia kuyayahudisha maeneo matukufu ya dini za Kiislamu na Kikristo yenye historia ndefu sambamba na kupotosha utambulisho wa maeneo hayo.
Tangu ilipoanza Intifadha ya Quds mwanzoni mwa mwezi Oktoba mwaka jana hadi sasa, zaidi ya Wapalestina 200 wameshauliwa shahidi na Wazayuni katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan, Ukanda wa Ghaza na Baytul Muqaddas.