Al-Abadi: Daesh haina nafasi katika ardhi ya Iraq
Haider al-Abadi, Waziri Mkuu wa Iraq amepongeza hatua ya kukombolewa kikamilifu mji wa kistratejia wa Fallujah toka mikononi mwa Daesh (ISIS) na kusema kuwa kundi hilo la kigaidi na kitakfiri halina nafasi katika nchi hiyo ya Kiarabu.
Akilihutubia taifa jana kupitia runinga ya dola, al-Abadi amesema kuwa kundi la Daesh halina nafasi katika taifa hilo na kwamba wanachama wake watazidi kushindwa na kusambaratishwa kwa kuwa wananchi wote wameungana dhidi yao. Amesema: "Tuliwaahidi kwamba tutaukomboa mji wa Fallujjah, hilo limewezekana, sasa tunawaahidi kuwa jeshi letu kwa kushirikiana na vikosi vya kujitolea vya wananchi viko mbioni kuukomboa mji wa Mosul ambao unatumiwa na Daesh kama makao makuu yake tokea Juni mwaka 2014." Haya yanajiri baada ya jeshi la Iraq na harakati ya wananchi ya Hashdu sh-Shabi, kuingia katika mji huo na kupeperusha bendera ya taifa hilo kwenye majengo ya serikali. Naibu mkuu wa baraza la harakati ya Hashdu sh-Shabi, Abu Mahdi al-Muhandis, katibu mkuu wa taasisi ya Badr, Hadi al-Amir na kamanda wa operesheni za kuukomboa mji huo, Abdul Wahab Al-Saidi, walimwandikia barua Waziri Mkuu wa Iraq, Haider al-Abadi wakimtaarifu juu ya mafanikio ya operesheni hizo. Hii ni katika hali ambayo, Jamhuri ya Kiislamu kupitia Hossein Jaberi Ansari, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imepongeza ushindi wa vikosi vya Iraq katika mji wa Fallujah. Taarifa ya msemaji huyo wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imesema kuwa, kuna matumaini kuwa Iraq itazidi kupata ushindi dhidi ya magenge ya kigaidi yanayoungwa mkono na Saudia, Marekani na utawala haramu wa Israel.