Nchi za Kiarabu zalaani mashambulizi ya wanajeshi wa Kizayuni huko Nablus
Baadhi ya nchi za Kiarabu zimelaani jinai mpya iliyotekelezwa na Maghasibu wa Kizayuni dhidi ya Wapalestina katika mji wa Nablus.
Wanajeshi wa utawala wa Kizayuni jana waliuvamia mji wa Nablus katika Ukingo wa Magharibi kwa kisingizio cha kuwatia nguvu raia wa Palestina; ambapo wanajeshi hao waliwafyatulia risasi raia wa Palestina na kuwauwa shahidi 10 na kuwajeruhi 102.
Kufuatia jinai hiyo, nchi za Kiarabu yaani Jordan, Misri, Saudi Arabia, Qatar, Kuwait, Oman, Imarati, Algeria pamoja na Uturuki zimetoa taarifa kwa nyakati tofauti zikilaani kile ilichokitaja kuwa hatua za wanajeshi ghasibu wa Kizayuni dhidi ya Wapalestina huko Nablus.
Nchi hizo tajwa aidha zimetangaza kuwa zinapinga kikamilifu hatua za wanajeshi wa Israel za kukiuka sheria za kimataifa na kuitolea wito jamii ya kimataifa kutekeleza majukumu yake ili kuhitimisha ukaliwaji mabavu na kukomesha mivutano na mashambulizi ya Israel dhidi ya Wapalestina.
Haki za wananchi madhlumu wa Palestina kwa zaidi ya miaka sabini sasa zimeghusubiwa chini ya ukandamizaji wa utawala wa Kizayuni. Utawala huo ghasibu unaoikalia Quds kwa mabavu katika kipindi chote hicho umetenda jinai za kikatili na kinyama zaidi dhidi ya Wapalestina.