Nasrullah: Matukio ya sasa yanaashiria hakika ya kusambaratika Israel
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i94822-nasrullah_matukio_ya_sasa_yanaashiria_hakika_ya_kusambaratika_israel
Katibu Mkuu wa Harakati ya Hizbullah ya Lebanon amesema matukio na maendeleo yanayoshuhudiwa hivi sasa katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu ni ishara tosha kuwa suala la kuporomoka kwa utawala wa Kizayuni wa Israel ni hakika ambayo itafanyika katika mustakabali wa karibu.
(last modified 2026-03-17T04:36:21+00:00 )
Mar 07, 2023 04:05 UTC
  • Nasrullah: Matukio ya sasa yanaashiria hakika ya kusambaratika Israel

Katibu Mkuu wa Harakati ya Hizbullah ya Lebanon amesema matukio na maendeleo yanayoshuhudiwa hivi sasa katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu ni ishara tosha kuwa suala la kuporomoka kwa utawala wa Kizayuni wa Israel ni hakika ambayo itafanyika katika mustakabali wa karibu.

Sayyid Hassan Nasrullah aliyasema hayo jana katika hotuba yake kwa njia ya televisheni kwa mnasaba wa maadhimisho ya kuwaenzi Mashahidi wa Hizbullah yaliyofanyika mjini Beirut na kusisitiza kuwa, maamuzi yote yaliyochukuliwa na mamlaka za Kizayuni yanaashiria kuwa Wazayuni wapo katika mkondo aa kuporomoka na kusambaratika.

Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon ameeleza bayana kuwa, mgawanyiko ndani ya utawala wa Kizayuni wa Israel, ni ishara ya kuongezeka kasi ya kusambaratika utawala huo pandikizi. 

Sayyid Nasrullah amesisitiza kuwa, mapambano na muqawama ndio njia pekee ya kuikomboa Palestina na Quds Tukufu inayokaliwa kwa mabavu na Wazayuni.

Amefafanua kwa kusema, "Maamuzi yanayochukuliwa na Wazayuni hayatakuwa na matokeo mengine ghairi ya kuzidisha ari, imani na subira ya Wapalestina ya kuendeleza operesheni zao za kulipiza kisasi."

Maandamano dhidi ya serikali ya Netanyahu

Katika sehemu nyingine ya matamshi yake Sayyid Nasrullah amelaani hatua ya serikali yenye misimamo ya kufurutu ada ya Benjamin Netanyahu ya kupasisha muswada ambao ukiidhinishwa na kuwa sheria, mamlaka za Kizayuni zitakuwa na kibali cha kuwaua wafungwa wa Kipalestina.

Amesema: Adui katili Mzayuni anadhani kuwa atawanyamazisha na kuwafumba midomo Wapalestina kwa kutishia wanajihadi na makundi ya muqawama au kuwahukumu kifo.

Sanjari na kutangaza uungaji mkono kwa wafungwa wa Kipalestina, Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon amesema umma wote wa Kiislamu una wajibu wa kuliunga mkono taifa la Palestina mkabala wa utawala wa Kizayuni.