Rais wa Palestina: Walimwengu chukueni hatua za kuzuia ugaidi wa Israel
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i94840-rais_wa_palestina_walimwengu_chukueni_hatua_za_kuzuia_ugaidi_wa_israel
Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina ameitaka jamii ya kimataifa kukomesha ugaidi wa Israel na kufanya juhudi za kuhitimisha uvamizi na ukaliaji ardhi kwa mabavu unaofanywa na utawala huo wa Kizayuni.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 07, 2023 22:53 UTC
  • Rais wa Palestina: Walimwengu chukueni hatua za kuzuia ugaidi wa Israel

Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina ameitaka jamii ya kimataifa kukomesha ugaidi wa Israel na kufanya juhudi za kuhitimisha uvamizi na ukaliaji ardhi kwa mabavu unaofanywa na utawala huo wa Kizayuni.

Mahmoud Abbas ametoa wito huo katika mkutano wa tano wa Umoja wa Mataifa unaohusu nchi zenye ukuaji wa chini zaidi kimaendeleo unaofanyika Doha, Qatar.

Abbas ameongeza kuwa, tangu miaka 75 iliyopita, wananchi wa Palestina wamekuwa wakiteseka kutokana na masaibu ya Nakba na maafa ya kuhamishwa kwa mabavu wakibaki bila makazi, na wanakabiliwa na jinai za uvamizi na kukaliwa ardhi zao kwa mabavu, jinai ambzo tangu mwaka 1967 zimegeuzwa kuwa ukoloni wa kudumu unaokiuka maazimio halali ya kimataifa na kutenda vitendo vya uangamizaji wa mbari.

Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina amebainisha kuwa, utawala ghasibu wa Israel unalenga kubadilisha utambulisho wa mji wa Baitul Muqaddas Mashariki unaoukalia kwa mabavu na unaendeleza ujenzi haramu wa vitongoji na mauaji ya Wapalestina.

Mahmoud Abbas

Mahmoud Abbas amesisitiza kuwa, magenge ya kigaidi ya walowezi wa Kizayuni yanachoma moto mali za Wapalestina wasio na ulinzi, kama ilivyotokea hivi majuzi katika eneo la Huwara, huku mawaziri wa Israel pia wakiwachochea kuua, kuharibu na kuliangamiza eneo hilo.

Hatua zinazochukuliwa na utawala haramu wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Wapalestina ni mifano hai ya ubaguzi wa Apathaidi, kwa sababu kifungu cha pili cha Mkataba wa Kimataifa unaopiga marufuku na kutoa adhabu kwa uhalifu wa ubaguzi wa Apathaidi kinasema: "jinai ya Apathaidi inahusu matendo yasiyo ya kiutu ambayo yanafanywa ili kuanzisha na kuendeleza utawala wa kundi la mbari moja dhidi ya kundi la mbari nyingine na kuwakandamiza watu wa kundi hilo kimpangilio".

Kwa zaidi ya miaka 75 sasa haki za wananchi wanaodhulumiwa wa Palestina zinaendelea kupondwa na kukandamizwa na utawala haramu wa Kizayuni wa Israel, ambao katika muda wote huo umefanya jinai za kinyama zaidi dhidi ya Wapalestina.../