Netanyahu ataka waandamanaji wakandamizwe na jeshi linalokaidi amri zake lichukuliwe hatua
-
Benjamini Netanyahu
Duru za lugha ya Kiibrania zimetangaza kuwa, Benjamini Netanyahu, Waziri Mkuu wa Israel ametoa wito wa kukandamizwa uasi wa jeshi la utawala huo haramu na kuchukuliwa hatua kali na thabiti zaidi dhidi ya waandamanaji wanaopinga serikali yake.
Siku ya Jumamosi, maelfu ya walowezi wa Kizayuni waliandamana kwa wiki ya 11 mfululizo kupinga mpango wa mageuzi ya mahakama unaosukumwa na kufuatiliwa kwa karibu na waziri mkuu huyo.
Kwa mujibu wa ripoti ya kanali ya Al-Mayadeen jana Jumatatu, Benjamin Netanyahu amekosoa vikali waandamanaji wanaopinga mpango wa serikali yake wa kubadilisha mfumo wa mahakama na kutaka hatua kali zichukuliwe dhidi yao ikiwa ni pamoja na makamanda wa jeshi, polisi na maafisa wa huduma ya usalama wa umma "Shabak".
Kwa mujibu wa taarifa, Netanyahu anavitaka vikosi vya usalama vichukue hatua zaidi katika kuingilia na kuzima maandamano ya raia wanaopinga serikali yake na wakati huo huo kuwataka makamanda wa vyombo vya usalama na mkuu wa majeshi kuchukua msimamo mkali zaidi dhidi ya waandamanaji na kukabiliana na uasi.
Kufuatia ombi hilo, viongozi wa upinzani, bila kupoteza wakati wamelaani matamshi hayo ya Netanyahu na kusema huenda yakachochea zaidi mgogoro unaoendelea ndani ya utawala huo ghasibu.
Uamuzi wa baraza la mawaziri la Benyamin Netanyahu wa kubadilisha mfumo wa mahakama wa utawala wa Kizayuni umeibua mivutano ya kisiasa na hitilafu kali kati ya muungano unaotawala na mrengo wa upinzani, na hivyo kuongeza maonyo kuhusu uwezekano wa kuibuka vita vya wenyewe kwa wenyewe miongoni mwa Wazayuni wanaokalia kwa mabavu ardhi za Wapalestina.