UN: Daesh inatumia mbinu ya ukatili wa ngono Iraq
Mwakilishi Maalumu wa Umoja wa Mataifa katika Masuala ya Kukabiliana na Ukatili wa Kijinsia amesema kuwa kundi la kigaidi la Daesh linatumia ukatili wa kingono kama mbinu ya kigaidi nchini Iraq.
Taarifa iliyotolewa na Zainab Hawa Bangura imesema kuwa, kwa sasa dunia inakabiliwa na tukio jipya ambapo ukatili wa kingono unatumiwa si kama mbinu ya kivita pekee bali pia mbinu ya kigaidi.
Taarifa hiyo ambayo imetolewa sambamba na Siku ya Kwanza ya Kimataifa ya Kukabiliana na Ukatili wa Kijinsia imesema kuwa, Umoja wa Mataifa una nia ya kutekeleza wajibu wake ili kuzuia migogoro inayohusiana na unyanyasaji wa kijinsia na kutoa huduma kwa waathirika.
Vilevile Bangura na Mwakilishi Maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Iraq, Jan Kubis wameeleza mshikamano wao na waathiri wa ukatili wa kingono unaofanywa na wapiganaji wa kundi la kigaidi la Daesh.