May 30, 2023 09:32 UTC
  • Haitham al Ghais
    Haitham al Ghais

Katibu Mkuu wa jumuiya ya nchi zinazozalisha mafuta kwa wingi Duniani (OPEC) amesema kuwa jumuiya hiyo inakaribisha kurejea kikamilifu Iran katika soko la mafuta baada ya kuondolewa vikwazo.

Shirika la habari la Tasnim limeripoti kuwa, Haitham al Ghais ameeleza kuwa Iran ni moja ya wanachama wa OPEC lakini uuzaji nje mafuta wa nchi hii ulikabiliwa na vizuizi kutokana na vikwazo vya Marekani. 

Katibu Mkuu wa OPEC ambaye anatazamia kufanya ziara mjini Tehran ameongeza kusema kuwa: Iran ina uwezo wa kuzalisha mafuta kwa kiwango kikubwa na kuingia katika masoko ya kimataifa katika kipindi kifupi. 

Haitham al Ghais vilevile ameashiria hatua ya nchi wanachama wa Jumuiya ya OPEC ya kupunguza kwa hiari uzalishaji mafuta na taathira zake kwa bei ya mafuta kimataifa na kueleza kuwa: Kunachukuliwa hatua na maamuzi kwa lengo la kuweka uwiano mzuri kati ya uuzaji mafuta na mahitaji ya bidhaa hiyo katika soko la dunia. 

Jumuiya ya Opec 

Saudi Arabia na nchi nyingine wanachama wa jumuiya ya OPEC+ katika hatua ya kushangaza, mwezi uliopita wa Aprili zilitangaza kwamba zingepunguza uzalishaji mafuta kwa mapipa mengine milioni 1.2. Kwa kupunguza kiwango hicho cha mapipa milioni 1.2 ya mafuta, nchi wanachama wa OPEC zitakuwa zimepunguza mapipa milioni 3.66 kwa siku katika uzalishaji wa OPEC+ .

Tags