NAM yasisitiza ulazima wa kulindwa haki za watu wa Palestina
Mawaziri wa mambo ya nje wa Vuguvugu la Nchi Zisizofungamana na Siasa za Upande Wowote (NAM), wameeleza katika taarifa ya mwisho ya mkutano ulofanyika katika mji mkuu wa Jamhuri ya Azerbaijan, Baku, kwamba kuna haja ya kufanyika juhudi zaidi kimataifa za kutafuta njia ya ufumbuzi wa kiuadilifu utakaohakikisha Wapalestina wanarejeshewa haki zao.
Mkutano wa mawaziri wa mambo ya nje na wawakilishi wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Nchi Zisizofungamana na Siasa za Upande Wowote ulifanyika tarehe 5 na 6 Julai ukiwa na kauli mbiu “Jumuiya ya Nchi Zisizofungamana na Siasa za Upande Wowote; Umoja na Uthabiti katika Kukabili na Changamoto Zinazojitokeza” katika mji wa Jamhuri ya Azerbaijan, Baku. Harakati ya Nchi Zisizofungamana na Siasa za Upande Wowote imekuwa ikilipa kipaumbele suala la Palestina tangu kuanzishwa kwake mwaka 1961. Kamati ya Palestina, ikiwa ni moja ya kamati tisa za shirika hilo la kimataifa, imekuwa ikikutana mara kwa mara tangu 1985, na wajumbe wake wanajadili masuala yanayohusiana na haki za Wapalestina katika mikutano mbalimbali. Mwaka huu, katika kikao cha Kamati ya Palestina ya NAM huko Baku, wanachama hao walijadili na kulaani mashambulizi ya utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya kambi ya wakimbizi wa Kipalestina ya Jenin. Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Hossein Amir Abdollahian aliyehutubia kamati hiyo, alisema: "Katika siku za hivi karibuni, tumeshuhudia jinai za utawala bandia wa Israel katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan, ambazo zimekabiliwa na mapambano makali ya wananchi na vijana wa Palestina. Kwa hakika suala la Palestina sio mzozo wa kisiasa au wa kieneo tu bali linaakisi thamani na mapambano ya wanamuqawama wanaopigania amani na haki zao za asili".
Washiriki wa mkutano wa Baku wamelaani mashambulizi yanayoongezeka ya jeshi la utawala ghasibu vya Israel na walowezi wa Kizayuni dhidi ya raia wa Palestina likiwemo shambulio la hivi karibuni katika kambi ya wakimbizi ya Jenin.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina, Riyad al-Maliki, pia alikuwepo katika mkutano huo ambako mawaziri wa mambo ya nje wa nchi tofauti, waliunga mkono suala la Palestina na mapambano ya Wapalestina.
Kwa upande wake, Fouad Hossein, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iraq amesema katika mkutano huo kuhusu kadhia ya Palestina kwamba: "Kuendelea jinai za utawala ghasibu wa Israel, ambazo zimepelekea kuuawa baadhi ya Wapalestina wasio na ulinzi katika mji wa Jenin, kunapaswa kulaaniwa. Fouad Hossein amesisitiza msimamo thabiti wa Iraq wa kuunga mkono mapambano ya Palestina."
Kwa ujumla ni kwamba, tunaweza kusema kuwa, dhati ya kupinga dhulma ya Jumuiya ya Nchi Zisizofungamana na Siasa za Upande Wowote ni fursa nzuri ya kupanga na kujadili suala la Palestina kadiri inavyowezekana ili kutetea haki za watu wa taifa hilo. Hata hivyo katika njia hiyo kuna vizuizi kadhaa, kama vile uhusiano wa karibu wa baadhi ya nchi wanachama wa jumuiya ya NAM na Utawala wa Kizayuni wa Israel, jambo ambalo pia limeashiriwa na Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ambayye amesema: "Tunalaani vikali mwingiliano wowote wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Nchi Zisizofungamana na Siasa za Upande Wowote na Utawala wa Kizayuni, ambao unaweza kuwa na athari mbaya za kisiasa, kiusalama, kijeshi, kijamii na kiuchumi kwa nchi nyingine wanachama wa harakati hiyo."
Hata hivyo, harakati za Kamati ya Palestina katika jumuiya kubwa zaidi ya kimataifa baada ya Umoja wa Mataifa yenye nchi wanachama 120, wanachama 20 waangalizi na jumuiya 10 za kimataifa, inaweza kuwa fursa nzuri ya kuangazia kadhia ya Palestina na kufuatilia suala la haki za Wapalestina. Katika fremu hii, ushirikiano wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Nchi Zisizofungamana na Siasa za Upande Wowote, hususan nchi za Asia, unapaswa kupanuliwa kwa kuzingatia haki, usalama na utulivu wa kikanda.