Kupigwa marufuku vazi la Abaya katika shule za umma nchini Ufaransa
https://parstoday.ir/sw/news/world-i101632-kupigwa_marufuku_vazi_la_abaya_katika_shule_za_umma_nchini_ufaransa
Katika miaka ya hivi karibuni, nchi za Magharibi zimeonyesha sera za chuki dhidi ya Uislamu na Waislamu katika nyanja mbalimbali za kisiasa na kijamii.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Aug 29, 2023 22:56 UTC
  • Kupigwa marufuku vazi la Abaya katika shule za umma nchini Ufaransa

Katika miaka ya hivi karibuni, nchi za Magharibi zimeonyesha sera za chuki dhidi ya Uislamu na Waislamu katika nyanja mbalimbali za kisiasa na kijamii.

Kuhusiana na hilo, Wizara ya Elimu ya Ufaransa, katika hatua yake ya hivi juzi  imepiga marufuku wasichana wa Kiislamu kuvaa abaya katika shule za umma nchini humu.

Waziri wa Elimu wa Ufaransa Gabriel Attal amesema kuwa, serikali ya nchi hiyo itapiga marufuku wanafunzi kuvaa abaya wakati wanapokuwa shule.

Katika mahojiano na shirika la habari la Ufaransa la TF1, waziri huyo ameeleza kuwa atafanya mazungumzo mapema wiki hii na wakuu wa shule za umma ili kuwasaidia kutekeleza marufuku hiyo.

Marufuku hiyo inatarajiwa kuanza kutekelezwa pindi tu muhula mpya wa masomo utakapoanza mnamo Jumatatu ijayo.

Waziri wa Elimu wa Ufaransa alipokuwa akitangaza kupiga marufuku uvaaji wa abaya kwa wasichana wenye stara katika shule za nchi hii, alidai eti abaya inakiuka sheria za kisekula za Ufaransa katika elimu.

Uamuzi huu unatangazwa katika hali ambayo, ripoti nyingi zinaonyesha kuwa, wasichana wa Kiislamu walipokea kwa wingi mno kuvaa abaya katika shule za Ufaransa. Kwa hakika, vazi la abaya ambalo linachukuliwa kuwa buibui la mtindo wa kisasa huvaliwa na baadhi ya wanawake wa Kiislamu kama stara na aina ya vazi, na sio vazi la kidini. Lakini mamlaka za Ufaransa zinalichukulia vazi hili kama ishara ya kidini na kulipiga marufuku.

Mwamko wa kuvaa hijabu barani Ulaya umeongezeka licha ya vikwazo na mibinyo mingi dhidi ya Waislamu

 

Katika kipindi cha chini ya mwaka mmoja uliopita, aliyekuwa Waziri wa Elimu wa Ufaransa Pap Ndiaye, alikataa kupiga marufuku uvaaji wa abaya, na katika kuelezea uamuzi wake kwa Seneti ya nchi hiyo alisema: "Ni vigumu sana kuamua kuhusu abaya kwa mujibu wa sheria." Kama uamuzi huu utapingwa katika mahakama ya idara, basi tutashindwa katika majadala wa kisheria.

Dawood Reifi, mhadhiri wa masomo ya Kiislamu katika Taasisi ya Mafunzo ya Kisiasa ya Lille Ufaransa anasema kuhusiana na hili: Hakuna kitu kinachoitwa mavazi ya Kiislamu peke yake. Lazima tuipe changamoto simulizi hii.

Hii si mara ya kwanza kwa viongozi wa Ufaransa kuchukua maamuzi dhidi ya mavazi ya Waislamu. Mwaka 2004 Ufaransa ilipiga marufuku wanawake kujifunga mitandio na vitambaa vya kichwa na mwaka 2010 ikapiga marufuku uvaaji wa niqabu. Si hayo tu, mwaka 2017 Ufaransa ilipasisha sheria kali ya kuwafuatilia Waislamu pamoja na kuwa na usimamizi mkali dhidi ya misikiti nchini humo.

Kama vile haitoshi, mwezi Juni mwaka huu Mahakama Kuu ya Utawala nchini Ufaransa ilitoa kibali kwa Shirikisho la Soka la nchi hiyo cha kupiga marufuku vazi la hijabu katika mashindano ya soka ya wanawake.

Makundi yenye chuki dhidi ya Uislamu yameendelea na kampeni zao

 

Kadhalika itakumbukwa kuwa, Januari mwaka jana (2022) Baraza la Seneti la Ufaransa lilipiga kura na kupasisha sheria inayopiga marufuku uvaaji wa vazi la stara na heshima la hijabu katika mashindano ya michezo.

Huko nyuma pia Baraza la Seneti la Ufaransa limewahi kupasisha mpango unaopiga marufuku wasichana wenye umri chini ya miaka 18 kuvaa Hijabu katika maeneo ya umma.

Tangu Rais Emmanuel Macron aliposhika hatamu za uongozi nchini Ufaransa, vitendo vya chuki dhidi ya Uislamu na hata kuvunjiwa heshima matukufu ya Uislamu vimeongezeka mno katika nchi hiyo ya bara Ulaya.

Viongozi wa Ufaransa, ambao wanadai uhuru na haki ya kuchagua kwa watu wote, katika miaka ya hivi karibuni wameshadidisha mashinikizo kwa jamii za walio wachache kimbari na kidini wakiwemo Waislamu. Viongozi wa Paris wanawawekea vikwazo na kuwatesa Waislamu kwa visingizio mbalimbali, kiasi kwamba, Waislamu wengi wameondoka Ufaransa. Ripoti ya utafiti ya Chuo Kikuu cha Lille ambayo ilitayarishwa baada ya kuwachunguza Waislamu 1,744 walioondoka Ufaransa inaonyesha kuwa, zaidi ya theluthi mbili ya watu hao waliripoti kwamba walihama kwa lengo la kuweza kutekeleza mambo yao ya kidini kwa uhuru kamili. Wakati huo huo, asilimia 70 walisema waliondoka Ufaransa ili kuepuka matukio ya kibaguzi dhidi yao.

Kwa hakika, Ufaransa, ambayo siku zote imekuwa ikipigia upatu uhuru wa mavazi, dini na kutoa maoni, filihali kwa kisingizio cha kutetea ubaguzi wa kidini, na kivitendio imebinya uhuru na kuweka mashinikizo dhidi ya jamii za walio wachache. Hii ni katika hali ambayo, makundi mengine ya kiraia kama vile watu wanaojihusisha na vitendo vya ngono za jinsia moja nchini Ufaransa wana uhuru kamili wa kufanya mambo yao pasi na kubughudhiwa.

Rais Emanuel Macron wa Ufaransa ambaye amekuwa akitangaza waziwazi misimamo yake ya chuki dhidi ya Uislamu na Waislamu

 

Wimbi la chuki dhiidi ya Uislamu halishuhudiwi nchini Ufaransa tu, bali hata katika mataifa mengine ya Ulaya hali ni hiyo hiyo. Madola ya Magharibi yakitekeleza siasa za kindumakuwili yamezipokonya uhuru jamii za wafuasi wa dini za walio wachache hususan Waislamu. Hii ni katika hali ambayo, makundi mengine ya raia yana ruhusa ya kuendesha harakati za kidini na kijamii kwa uhuru kamili.

Hivi karibuni Martha Bissmann, mbunge wa zamani wa Bunge la Austria, akipinga pendekezo la kupigwa marufuku vazi la Hijabu nchini humo alisema: “Mnataka kuwaadhibu wanawake wa Kiislamu, wanawake ambao miongoni mwao kuna madaktari, walimu, wanasayansi na wafanyakazi? wao ni wanawake na mabinti waliofanikiwa sana katika jamii.

Hivi sasa uamuzi wa Ufaransa wa kuweka vikwazo vya kuvaa abaya kwa wasichana wa shule umeonyesha mkanganyiko wa maneno na matendo ya nchi za Magharibi; hasa viongozi wa kisiasa wa mataifa haya, wakiwemo viongozi wa Ufaransa, ambao wamekuwa mstari wa mbele kukosoa nchi zingine kwa kujaribu kuweka mibinyo ya mavazi na wanatoa taarifa dhidi ya nchi kama hizo.