Nov 25, 2023 11:47 UTC
  • Uhispania na Ubelgiji zatangaza kuwa tayari kuitambua rasmi nchi ya Palestina

Hatua ya Uhispania na Ubelgiji ya kutangaza kuwa tayari kuitambua rasmi nchi huru ya Palestina ni tukio muhimu kushuhudiwa barani Ulaya kuhusu kadhia ya Palestina. Hatua hii imeukasirisha sana utawala wa Kizayuni.

Pedro Sanchez Waziri Mkuu wa Uhispania na Alexander De Croo mwenzake wa Ubegiji ambao kwa pamoja walifanya ziara fupi huko Misri wamelaani jinai za utawala wa Kizayuni dhidi ya wakazi wa Ukanda wa Gaza. Pedro Sanchez Waziri Mkuu wa Uhispania jana Ijumaa alieleza kuwa Madrid ipo tayari kuitambua rasmi kwa upande mmoja nchi ya Palestina hata kama hatua hiyo itapingana na mtazamo wa Umoja wa Ulaya. 

Jinai za Israel Ukanda wa Gaza 

Sanchez amewaambia waandishi wa habari katika mkutano wa vyombo vya habari uliofanyika katika kivuko cha Rafah huko Misri kwamba anadhani wakati umefika sasa kwa jamii ya kimataifa hasa Umoja wa Ulaya na nchi wanachama wa umoja huo kuitambua nchi ya Palestina. Waziri Mkuu wa Uhispania ambaye amechaguliwa hivi karibuni na kabla ya hapo aliwahi kusema kuwa anatoa kipaumbele kwa suala la kuitambua rasmi nchi ya Palestina ameongeza kuwa: "kama haitakuwa hivyo  Uhispania itafanya maamuzi yake yenyewe." 

Alexander De Croo Waziri Mkuu wa Ubelgiji pia amesema katika mahojiano na waandishi wa habari kuwa kipaumbele cha kwanza ni kuachiwa huru mateka wanaoshikiliwa na Hamas na kupunguza maafa ya binadamu huko Ukanda wa Gaza. De Croo amesema: Baada ya hatua hiyo tunapasa kuketi katika meza ya mazungumzo na kujadili suala la kuitambua rasmi Palestina. Uhispania hivi sasa ni Mwenyekiti wa Baraza la Umoja wa Ulaya na Ubelgiji itachukua nafasi hiyo kuanzia mwezi ujao wa Disemba; na kwa msingi huo kuwepo viongozi wa nchi mbili hizo huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu kumefanyika kwa lengo la kuwasilisha msimamo wa Umoja wa Ulaya. 

Mawaziri Wakuu wa Uhispania na Ubelgiji huko Rafah, Misri 

Kufuatia matamshi hayo, Wizara ya Mambo ya Nje ya utawala wa Kizayuni jana Ijumaa iliwaita kuwahoji mabalozi wa Uhispania na Ubelgiji na kudai kuwa matamshi ya Mawaziri Wakuu wa Uhispania na Ubelgiji ni ya kuunga mkono ugaidi. Taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje ya utawala wa Kizayuni imeeleza kuwa: "Tunalaani matamshi yasiyo sahihi ya viongozi wa serikali za Uhispania na Ubelgiji yanayounga mkono ugaidi." Benjamin Netanyahu Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni pia ametoa radiamali yake katika vyombo vya habari baada ya matamshi  ya Sanchez na De Croo kwa kusema: "Nalaani matamshi ya Mawaziri Wakuu wa Ubelgiji na Uhispania kwa kutoiwajibisha Hamas kwa jinai."  

Kukasirishwa pakubwa utawala wa Kizayuni na msimamo wa nchi mbili hizo muhimu za Umoja wa Ulaya kuhusu kuitambua rasmi nchi ya Palestina kunapata maana kwa kuzingatia matukio ya karibuni katika vita vya Gaza. Baada ya oparesheni ya Kimbunga cha Al Aqsa Oktoba 7 mwaka huu, viongozi wa utawala wa Kizayuni hasa Benjamin Netanyahu walitishia kuwa vita vitaendelea huko Gaza hadi kuangamizwa kikamilifu harakati ya Hamas. Pamoja na hayo, baada ya kupita karibu siku 50 za mashambulizi makubwa ya kikatili na ambayo hayajawahi kushuhudiwa tena ya anga ambayo yamewauwa shahidi na kujeruhi maelfu ya Wapalestina wakazi wa Ukanda wa Gaza na pia mashambulizi ya ardhini ya utawala huo ghasibu dhidi ya eneo hilo, lakini kufuatia kushindwa utawala wa Kizayuni kutimiza malengo yake iliyoyakusudia na pia kupata maafa makubwa ya kiroho na hasara nyingi kwa upande wa silaha na zana za kijeshi ikiwa ni pamoja na kulemewa na mashinikizo ya jamii ya kimataifa, Tel Aviv hatimaye imelazimika kukubali kusitisha vita kwa siku nne na kubadilishana mateka na Hamas. Kuuawa na kujeruhiwa makumi ya maelfu ya Wapalestina kumepelekea kupoteza maana ile taswira ya Israel kujifanya kuwa mdhulumiwa ambayo ilikuzwa sana na kupigiwa propaganda na vyombo vya habari vya Magharibi baada ya operesheni ya Kimbunga cha Al-Aqsa; na kwa mara nyingine tena kuibuliwa suala la utawala wa Kizayuni kukataa kutekeleza mpango wa serikali mbili licha ya kuukubali mpango huo huko nyuma. 

Kimbunga cha Al Aqsa 

Suala muhimu hapa ni kuwa licha ya uungaji mkono wa pande zote wa Wamagharibi wakiwemo viongozi wa Ujerumani, Uingereza na Ufaransa pamoja na Rais wa Marekani kwa Israel na jinai za utawala huo huko Ukanda wa Gaza kwa kisingizio cha kujilinda lakini hata wao pia wamekiri katika matamshi yao kuhusu kukataa utawala wa Kizayuni  mpango wa kuasisi dola mbili na wametaka kutekelezwa mpango huo. Ingawa serikali mbalimbali za utawala wa Israel zimekuwa zikipinga wazi mpango huo wa serikali mbili, lakini tangu kuundwa kwa baraza la mawaziri la mrengo wa kulia chini ya uongozi wa Benjamin Netanyahu Januari mwaka huu upinzani kwa suala hilo umeongezeka na hata baadhi ya mawaziri wake wanataka kufukuzwa na kuuawa Wapalestina kwa umati. Misimamo hii imewaweka waitifaki wa nchi za Magharibi wa utawala wa Kizayuni katika hali ngumu na hivyo hawana  njia ya kuhalalisha maamuzi na vitendo vya Israel. Nchi mbalimbali duniani na Umoja wa Mataifa zinataka kutekelezwa mpango wa serikali mbili na katika mkondo huo  nchi za Ulaya kama Uhispania na Ubelgiji pia zinataka kivitendo kuasisiwa nchi ya Palestina. 

Inaonekana kuwa suala la kuwaunga mkono Wapalestina na kuulaani utawala wa Kizayuni limekuwa gumzo kubwa duniani kote. Kwa hakika, kutokana na kubadilika taratibu ya mfumo wa kimataifa na kuwa wa kambi kadhaa; mazungumzo ya Wazayuni wa Magharibi kuhusu kadhia ya Palestina hayana tena nafasi, bali mwekeleo mpya unachukua nafasi hatua kwa hatua  juu ya ulazima wa kuheshimiwa haki za wananchi wa Palestina ikiwemo haki yao ya kuunda taifa huru la Palestina.

Tags