Mkuu wa Sera za Nje wa EU ataka upelekaji silaha kwa Israel ukomeshwe ili kupunguza maafa Gaza
Mkuu wa Sera za Nje wa Umoja wa Ulaya ametoa wito kwa washirika wa utawala wa Kizayuni Israel kukomesha upelekaji silaha kwa utawala huo ghasibu iwapo wanataka kupunguza vifo vya raia vinavyosababishwa na vita vyake vya mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina wa Ukanda wa Gaza.
Borrell ameeleza kuwa, ni kuonyesha mgongano kwa nchi kutangaza mara kwa mara kwamba Israel inaua raia wengi mno, lakini hazichukui hatua yoyote madhubuti kuzuia mauaji hayo.
"Kama jamii ya kimataifa inaamini kuwa haya ni mauaji, na kwamba watu wengi sana wanauawa, labda tunapaswa kufikiria kuhusu utoaji wa silaha [kwa Israel]", ameongezea kusema afisa huyo mwandamizi wa EU.
Ifahamike kuwa Marekani, ambayo ni mshirika mkubwa zaidi wa Israel, huupatia utawala huo wa Kizayuni msaada wa kijeshi wa dola bilioni 3.8 kila mwaka. Aidha, tangu Oktoba 7,2023 Washington imeipatia Tel Aviv silaha zaidi ya tani 10,000 pale utawala huo haramu ulipoanzisha vita vyake vya mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina wa Gaza.
Mashambulizi hayo ya kikatili ya kijeshi hadi sasa yameshateketeza roho za Wapalestina zaidi ya 28,300, wengi wao wakiwa wanawake na watoto, na kuwajeruhi wengine zaidi ya 67,900.../