Feb 20, 2024 07:06 UTC
  • Nchi 26 kati ya 27 za EU zataka 'kusitishwa vita haraka kwa sababu za kibinadamu' Ghazza

Mkuu wa Sera za Nje wa Umoja wa Ulaya Josep Borrell ametangaza kuwa, nchi zote wanachama wa umoja huo isipokuwa moja tu, ambazo ni 26 kati ya 27, zimetoa wito wa "kusitishwa mara moja mapigano huko Ghazza kwa sababu za kibinadamu", usitishaji ambao utapelekea kupatikana usitishaji wa kudumu wa vita katika eneo hilo.

Katika mkutano aliofanya na waandishi wa habari mjini Brussels, Borrell amesema nchi hizo wanachama 26 wa EU zimetilia mkazo pia uungaji mkono wao kwa taarifa yao ya awali inayoitaka serikali ya Israel ijizuie kuanzisha operesheni za kijeshi dhidi ya Rafah, ambayo zimeitaja kama mji wa "kimbilio la mwisho" kusini mwa Ghazza.
 
Borrell hakutaja nchi inayopingana na EU, lakini Hungary ilizuia taarifa kama hiyo siku chache zilizopita.
 
Wapalestina wapatao milioni 1.5 waliokimbia makazi yao baada ya mashambulizi ya kinyama ya utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Ghazza wamejificha mjini Rafah wakitafuta hifadhi ili kujinusuru na hujuma hizo za jeshi katili la Israel.
 
Mipango iliyoripotiwa na Israel ya kushambulia mji huo imeibua kelele za jamii ya kimataifa, huku nchi nyingi zikitaka kuzuiwa au kufutwa operesheni hiyo.
 
Kwa mujibu wa Borrell, nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya zimehimiza kuwepo usitishaji haraka wa mapigano kwa sababu za kibinadamu, usitishaji ambao utapelekea kutekelezwa usitishaji vita wa kudumu, kuachiliwa mateka bila masharti na kutolewa misaada ya kibinadamu; na wakati huohuo serikali ya Israel kutochukua hatua za kijeshi huko Rafah kwa sababu kutazidisha hali mbaya ya kibinadamu iliyopo na kuzuia kukidhiwa mahitaji ya haraka ya huduma za msingi na misaada ya kibinadamu inayohitajika huko Ghazza.
Josep Borrell

Mkuu wa Sera za Nje wa EU amethibitisha pia kuwa umoja huo unaangalia hatua madhubuti zinazopasa kuchukuliwa dhidi ya walowezi wa Kizayuni wenye itikadi kali ambao wanashambulia kiholela raia wa Palestina katika Ukingo wa Magharibi.

 
Israel ilianza kufanya mashambulizi makali na ya kinyama katika Ukanda wa Ghazza kufuatia operesheni ya Kimbunga cha Al-Aqsa iliyotekelezwa na harakati ya Hamas mnamo Oktoba 7, 2023. Mashambulio hayo ya mabomu na makombora yaliyofanywa na utawala haramu wa Israel yameua shahidi zaidi ya Wapalestina 29,000 na kujeruhi zaidi ya 69,000 mbali na kusababisha uharibifu mkubwa na uhaba mkubwa wa mahitaji ya msingi.
 
Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, vita vya utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Ghazza vimesababisha pia asilimia 85 ya wakazi wa eneo hilo kuhama makazi yao huku kukiwa na uhaba mkubwa wa chakula, maji safi na dawa, na asilimia 60 ya miundombinu ya eneo hilo kuharibiwa au kubomolewa kikamilifu.
 
Utawala wa kibaguzi na wa Kizayuni wa Israel umeshtakiwa katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki kwa kufanya mauaji ya kimbari. Uamuzi wa muda uliotolewa na mahakama hiyo mwezi Januari uliiamuru Tel Aviv kusitisha vitendo vya mauaji ya kimbari na kuchukua hatua za kuhakikisha misaada ya kibinadamu inatolewa kwa raia huko Ghazza.../

 

Tags