Jul 10, 2016 03:40 UTC
  • Misikiti London yapokea vitisho kutoka magaidi wa mrengo wa kulia

Misikiti kadhaa mjini London Uingereza imepokea vitisho vya kigaidi kutoka kwa makundi yanayoaminika kuwa ya wabaguzi wa mrengo wa kulia huku vitendo vya chuki dhidi ya Uislamu vikiongezeka nchini humo.

Taarifa zinasema misikiti kadhaa mjini London imepokea vifurushi vyenye poda nyeupe huku kukiwa na maandishi ya kibaguzi dhidi ya Waislamu jambo ambalo limepelekea idara ya kupambana na ugaidi nchini humo kuanzisha uchunguzi.

Vifurishi hivyo vilitumwa Alhamisi katika misikiti mitatu ya Masjid Ayesha Tottenham, Masjid Noor ul Islam Leyton na Masjid Finsbury Park yote ya mjini London.

Kifurushi kimoja pia kilitumwa kwa Lord Nazir Ahmed ambaye ni mjumbe katika Bunge la Malodi la Uingereza ambaye pia alipokea matusi katika kifurushi chake.

Maafisa wa misikiti hiyo walilazimika kuvalia mavazi maalumu wakati uchunguzi ukifanyika ambapo misikiti hiyo pia ilifungwa kwa muda.

Tokea Waingereza wapige kura ya kujiondoa Umoja wa Ulaya maarufu kama Brexit Juni 23, Waislamu Uingereza wanakabiliana na ongezeko la chuki dhidi ya Uislamu ambapo wanawake wanaovaa Hijabu ndio wanaoathirika zaidi.

Baraza la Waislamu Uingereza limesema kulijiri hujuma 100 za chuki dhidi ya Waislamu katika wikendi ya kwanza kufuatia kura hiyo ya maoni. Katibu Mkuu wa Baraza la Waislamu Uingereza Shuja Shafi ametahadharisha kuhusu vitendo vya kushtua vya chuki dhidi ya Waislamu na jamii za waliowachache nchini humo na ameitaja hali hiyo kuwa mgogoro wa sasa unaohatarisha amani ya kijamii.

Ugaidi wa mrengo wa kulia unaongezeka kwa kasi na unachochewa na itikadi za wazungu wa mrengo wa kulia wenye misimamo mikali ambao wanapinga watu wasiokuwa wazungu na hasa Waislamu. Ugaidi wa aina hii unapuuzwa na jamii ya kimataifa huku Waislamu wakiendelea kuwa waathirika wakuu.

 

Tags