Mar 06, 2024 02:14 UTC
  • Indhari ya asasi za kimataifa kuhusu kushtadi njaa na umasikini nchini Afghanistan

Kupungua kwa misaada ya kimataifa nchini Afghanistan kumepelekea kushadidi umaskini na njaa katika nchi hiyo.

Katika ripoti yake, Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) limeeleza kuwa, kuna watoto na akina mama milioni nne wanaokabiliwa na utapiamlo nchini Afghanistan ambao umezidishwa na umaskini na njaa katika nchi hiyo kutokana na kupunguzwa kwa misaada. Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Misaada ya Kibinadamu (OCHA) imetangaza kuwa, mipango mingi ya misaada nchini Afghanistan inakabiliwa na mkwamo kutokana na ukata na uhaba wa bajeti. OCHA imeongeza kuwa, kati ya dola bilioni 3.6 zinazohitajika kwa ajili ya msaada nchini Afghanistan mwaka huu, ni dola milioni 87 pekee ndizo zimetolewa hadi sasa.

Hapo awali, Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Misaada ya Kibinadamu ilisema kuwa, kutokana na ukosefu wa usawa na udhaifu uliopo, ikiwa ni pamoja na ukosefu wa huduma za kijamii na afya, Afghanistan inakabiliwa na mgogoro mkubwa wa kibinadamu.

Kwa mujibu wa takwimu za Umoja wa Mataifa, zaidi ya theluthi moja ya watu milioni 40 wa Afghanistan wanakabiliwa na ukosefu wa chakula. Antonio Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amethibitisha kuwa, umoja huo hadi sasa umetoa sehemu ndogo tu ya bajeti inayohitajika ili kukabiliana na mgogoro wa kibinadamu nchini Afghanistan.

Watoto wa Afghanistan wakipata chakula cha msaadaa

 

Hii si mara ya kwanza kwa taasisi za kimataifa zikiwemo zile zenye uhusiano na Umoja wa Mataifa kuonya kuhusu kuzorota kwa usalama wa chakula nchini Afghanistan na kushadidi mzozo wa njaa kwa mamilioni ya watu nchini humo. Baada ya Taliban kushika tena hatamu za uongozi nchini Afghanistan mnamo Agosti 2021, mambo mbalimbali yalisababisha usalama wa chakula kuhatarishwa hatua kwa hatua katika nchi hiyo. Kuzuiwa kwa takriban dola bilioni 10 mali ya Afghanistan na serikali ya Marekani kwa kisingizio cha kuingia madarakani wanamgambo wa Taliban na kupungua uwezo wa kifedha wa kundi hilo wa kuagiza chakula kutoka nje kulipelekea kushuka kwa kiasi kikubwa kwa viashiria vya kiuchumi nchini Afghanistan, bei ya bidhaa muhimu na za kimsingi, na pia kupunguzwa sana au kukatwa kabisa misaada ya kimataifa ni moja ya sababu kuu za nchi hiyo kukabiliwa na tatizo la njaa na hivyo kuhatarisha usalama wa chakula.

Katika mazingira haya, serikali ya Taliban haijatoa mwanya wa kupunguzwa mashinikizo ya kimataifa dhidi ya Afghanistan kutokana na kung'ang'ania misimamo yake na utekelezaji wa sera za mibinyo ikiwa ni pamoja na kupiga marufuku wanawake kufanya kazi na mashirika yasiyo ya kiserikali.

Kwa hakika, majimui ya mashinikizo ya nje na ya ndani yameiweka Afghanistan katika kundi la nchi saba ambazo raia wake wanakabiliwa na baa la njaa na umaskini mkubwa.

Wanamgambo wa Taliban

 

 Afghanistan imewekwa katika orodha ya nchi maskini na zenye njaa katika hali ambayo, kutokaana na muundo na asili ya watu wake katika kilimo na ufugaji, endapo kutaandaliwa mipango kidogo ya kiakili katika sekta ya kilimo inaweza kwa urahisi sio tu kukidhi mahitaji yake ya chakula, lakini pia kuwa ghala la nafaka la eneo hili.

Wengi wanaamini kwamba, uendelezaji wa kilimo mbadala badala ya kasumba, ambao ulipendekezwa na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran zaidi ya miongo miwili iliyopita, bado ni suluhisho bora zaidi la kuiokoa kichakula Afghanistan kutokana na mgogoro mbaya wa sasa inaokabiliwa nao.

Kwa hivyo, inaonekana kwamba kuundwa serikali imara nchini Afghanistan na kuimarisha umoja wa kitaifa na kuibua harakati kubwa katika sekta ya kilimo na viwanda ndio njia pekee ya kuinasua Afghanistan kutoka katika hali ya sasa.

Vyovyote iwavyo, kutokana na kutokea mgogoro wa chakula nchini Afghanistan, khiyana na jinai za serikali zilizopita na wavamizi dhidi ya watu wa nchi hiyo zinadhihirika zaidi na inaonekana kwamba, serikali za nchi za Magharibi na asasi zao zinazofungamana nazo hazichukui hatua zozote za maana kusaidia kutatua matatizo ya chakula ya watu wa Afghanistan. Kwa muktadha huo, katika mazingira kama haya ili kung'oa mzizi wa tatizo la njaa na umaskini nchini Afghanistan, wananchi na maafisa wa nchi hiyo wanaweza sambamba na kutatua mizozo na mapigano yasiyo na natija, wataraji uungaji mkono wa kieneo, hususan Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC), kusaidia kutatua matatizo ya chakula na kumaliza mgogoro huo.

Tags