Mar 26, 2024 02:09 UTC
  • Undumakuwili wa Marekani kuhusiana na utawala wa Kizayuni na vita vya Gaza

Marekani, ikiwa ni mshirika muhimu zaidi na muungaji mkono asiye na masharti wa utawala wa Kizayuni wa Israel, inatekeleza sera ya undumakuwili kuhusu utawala huo na jinai zake. Kwa upande mmoja, katika kitendo cha kuonyesha mshikamano na Israel, Washington imetangaza msaada mpya wa kijeshi kwa utawala huo sambamba na kukata misaada kwa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi Wapalestina UNRWA.

Katika upande mwingine utawala wa Rais Joe Biden umedai unapinga mpango wa utawala wa Isael wa kushambulia eneo la Rafah lenye idadi kubwa ya wakimbizi wa Kipalestina huko Gaza.

Marekani imekata misaada yake kwa UNRWA  wakati jinai zinazoendelea za utawala wa Kizayuni katika Ukanda wa Gaza zimesababisha njaa na ukosefu wa chakula katika eneo hilo na hivyo kupelekea hali ya Wapalestina kuwa mbaya zaidi.

Msaada mpya wa kijeshi wa Marekani kwa Israel una thamani ya dola bilioni 3.8 kutoka dola bilioni 886 za bajeti ya Wizara ya Ulinzi ya Marekani.

Msaada huo mpya wa kijeshi wa Marekani kwa utawala wa Israel umetolewa katika fremu ya sera ya uungaji mkono wa kudumu kwa Tel Aviv. Msaada huo unakuja pamoja na kuwepo malamiko makali ya kimataifa kutokana na Israel kuendeleza vita vya mauaji ya kimbari dhidi ya Gaza na matumizi ya njaa kama silaha ya vita. Wakati huo huo, jinai zaidi za kivita za Israel zinaedenlea kufichuka. Imebainika kuwa askari katili wa Israel wamewabaka wanawake wa Kipalestina na kisha kuwaua wakiwa katika hospitali ya As Shifaa ya Gaza.

Katika upande mwingine, kusitishwa misaada ya Marekani kwa UNRWA kutaleta mshtuko mkubwa kwa shirika hilo la Umoja wa Mataifa lenye jukumu la kutoa misaada kwa Wapalestina wakiwemo wa Ukanda wa Gaza. Marekani na waitifaki wake wa Magharibi wamedai kuwa baadhi ya wafanyakazi wa UNRWA ni wapiganaji wa HAMAS bila kutoa ushahidi wowote. Harakati ya Hamas pia imekanusha vikali kuwa wapiganaji wake ni wafanyakazi wa UNRWA.

Biden na Netanyahu

Bila shaka, maafa makubwa yataibuka Gaza baada ya kupunguzwa misaada kwa UNRWA.

Watu Gaza wanakabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula na mahitaji ya kimsingi ya kibinadamu kutokana na vita na kuzingirwa na utawala wa Kizayuni wa Israel na hivyo kukosekana misaada kutafanya hali iwe mbaya zaidi kuliko ilivyo hivi sasa.

Utawala wa Kizayuni umekaidi matakwa ya kimataifa ya kusitisha jinai zake huko Gaza lakini pamoja na hayo Marekani ambayo ni muitifake wake mkuu imetoa tu onyo la kimaonyesho kwa utawala huo na imekataa kutumia uwezo wake wa kisiasa kuilazimisha Israeli isitishe vita na jinai dhidi ya Wapalestina..

Nukta muhimu ni kwamba mtazamo wa upendeleo wa utawala wa Biden kwa utawala wa Kizayuni wa Israel umekabiliwa na hisia nyingi pinzani ndani ya Marekani. Kuhusiana na suala hilo, idadi kubwa ya wafanyakazi wa serikali ya Marekani wanapanga kujiuzulu kutokana na vita vya Gaza na pia kama njia ya kuonyesha upinzani wao kwa uungaji mkono wa serikali yake kwa utawala katili wa Isarel. Awali, wafanyakazi mia moja wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani katika ujumbe maalumu walisema utawala wa Kizayuni umefanya jinai za kivita huko Gaza. Aidha zaidi ya wafanyakazi 700 wa idara mbali mbali za serikali ya Marekani, zikiwemo idara za usalama, mwezi Novemba walimwandikia barua Biden wakimtaka aunge mkono usitishaji mapigano Gaza.

Ni wazi kuwa mbali na wananchi waliowengi Marekani ambao wanakosoa vikali sera ya serikali ya Biden kuhusu vita vya Gaza kwa kujitokeza katika maandamano ya kuunga mkono Palestina, ukosoaji huo sasa umeenea hadi ndani ya serikali yenyewe ya Marekani.

Tags