Mar 26, 2024 10:52 UTC
  • Guterres atoa wito kwa nchi za Magharibi kulipa fidia Waafrika kutokana na biashara ya utumwa

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametoa wito wa kulipwa fidia watu waliosafirishwa kwa njia haramu kama watumwa kutoka Afrika hadi katika nchi za Bahari ya Atlantiki.

Katika taarifa yake kwa mnasaba wa Siku ya Kimataifa ya Kuwakumbuka Wahasiriwa wa Utumwa na Biashara ya Utumwa katika Bahari ya Atlantiki, Guterres amesema utumwa "uliweka misingi ya ubaguzi wa kikatili unaozingatia utawala wa Wazungu ambao bado unaendelea hadi leo."

Kuanzia karne ya 15 hadi 19, Waafrika wasiopungua milioni 12.5 walitekwa nyara, wakasafirishwa kwa lazima kwa meli na wafanyabiashara Wazungu wa Ulaya, na kuuzwa utumwani. Wale walionusurika safari hiyo ya kikatili waliishia kuhangaika kwenye mashamba ya Amerika, hasa Marekani, Brazil na Karibea.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema: "Wengi wa wale waliopanga na kuendesha biashara ya utumwa katika Bahari ya Atlantiki walijikusanyia utajiri mkubwa. Wakati huo huo, watumwa walinyimwa elimu, huduma za afya, fursa na ustawi."

Njia ya Biashara ya Utumwa katika Bahari ya Atlantiki

Kulingana na Guterres, maisha ya wale waliofanywa watumwa "yalitawaliwa na ugaidi," kwani walibakwa, kuchapwa viboko, na kukabiliwa na ukatili na udhalilishaji mwingine.

Septemba iliyopita, ripoti ya Umoja wa Mataifa ilipendekeza kwamba mataifa yafikirie kutoa fidia za kifedha kama njia ya kurekebisha dhuluma za utumwa.

Leo utajiri wa Marekani na nchi nyingi za Ulaya hasa Uingereza, Uholanzi na Uhispania unatokana na faida zilizopatikana wakati wa biashara ya utumwa na kwa msingi huo nchi hizo sasa zinatakiwa kulipa fidia kwa nchi za Kiafrika kutokana na biashara hiyo haramu.