Mar 27, 2024 12:25 UTC
  • Wachunguzi wa Russia kujadili ombi la kuchunguza kuhusika Magharibi katika ugaidi

Wachunguzi wa serikali ya Russia leo wameeleza kuwa watajadili ombi lililowasilishwa na wabunge waliotaka kuchunguzwa kile walichokiita kama "taasisi, ufadhili na vitendo vya ugaidi vinavyofanywa na Marekani na nchi nyingine za Magharibi dhidi ya Russia."

Mkurugenzi wa Shirika la Usalama la Russia amesema kuwa anaamini kuwa Ukraine pamoja na Marekani na Uingereza zimehusika katika hujuma ya kigaidi katika ukumbi wa tamasha nje ya jiji la Moscow iliyoua watu wasiopungua 139. 

Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Uingereza David Cameron alituma ujumbe katika mtandao wa kijamii wa X uliosomeka: "Madai ya Russia kuhusu Magharibi na Ukraine kuhusika katika hujuma ya Crocus City ni upuuzi mtupu."

Kundi la kigaidi la Daesh (ISIS) lilitangaza kuhusika na shambulio hilo la Moscow huku Washington na Paris zikisema kuwa zina taarifa za kiitelijinsia zinazothibitisha kuwa kundi hilo la kigaidi limehusika na hujuma hiyo. 

Russia kwa upande wake imetilia shaka madai ya Marekani kwamba kundi la kigaidi la Daesh (ISIS) limehusika na shambulio kwenye ukumbi wa tamasha nje ya jiji la Moscow ambapo tayari mahakama ya Moscow imewafungulia mashtaka wahusika wa shambulio hilo ambao walikamatwa kwa tuhuma za ugaidi.