Apr 17, 2024 10:48 UTC
  • NYT yaagiza waandishi wake: Msitumie misamiati ya 'mauaji ya kimbari', 'uangamizaji wa kizazi' katika vita vya Israel

Taasisi ya uchunguzi wa taarifa za mitandaoni nchini Marekani ya Intercept imefichua kuwa gazeti la New York Times limewaagiza waandishi na maripota wake wa habari wanaoripoti vita vya mauaji ya kimbari yanayofanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Wapalestina wa Ukanda wa Ghaza, wajizuie kutumia misamiati ya "mauaji ya kimbari" na "uangamizaji wa kizazi" na kupeuka kutumia neno “eneo linalokaliwa kwa mabavu” kumaanisha ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na Israel.

Intercept imenasa nakala ya memo ya ndani, iliyotolewa na New York Times ambayo imewaagiza pia wanahabari na maripota wake kutotumia neno Palestina "isipokuwa kwa nadra katika matukio machache sana".

Memo hiyo iliyoandikwa na mhariri wa viwango wa gazeti la New York Times Susan Wessling, mhariri wa kimataifa Philip Pan, na manaibu wao imewataka pia waandishi wa habari kuachana na neno "kambi za wakimbizi" kuelezea maeneo ya Ghaza ambayo kihistoria yalikaliwa na Wapalestina waliofukuzwa kutoka maeneo mengine ya Palestina wakati wa vilivyopita baina ya utawala wa Kizayuni wa Israel na Waarabu.

Waungaji mkono wa Palestina wakiandamana mbele ya ofisi za New York Times

Umoja wa Mataifa unayatambua maeneo hayo kama kambi za wakimbizi zinazohifadhi mamia ya maelfu ya wakimbizi waliosajiliwa.

Kwa mujibu wa Intercept, waandishi wa gazeti hilo maarufu nchini Marekani wamesema, waraka huo unatoa mwongozo kuhusu baadhi ya masharti na masuala mengine ambayo wamekabiliana nayo tangu kuanza kwa mzozo wa Ghaza mwezi Oktoba.

Wafanyakazi kadhaa wa New York Times wameiambia The Intercept kwamba, memo hiyo inathibitisha wazi kuwa gazeti hilo linafuata simulizi za upendeleo na upotoshaji zinazotolewa na Israel.

Mfanyakazi mmoja wa chumba cha habari katika gazeti la New York Times ambaye hakutaka jina lake litajwe ameielezea hali hiyo kuwa ni aina ya kitu ambacho kinaonekana kidhahiri kuwa ni cha  kitaalamu na kimantiki ikiwa mtu hajui muktadha sahihhi wa kihistoria wa mzozo wa Palestina na Israel. Lakini kama anajua, itamdhihirikia wazi kwamba, taarifa za gazeti hilo ni za kuupendelea utawala wa Kizayuni.../

Tags