Apr 27, 2024 03:34 UTC
  • Marekani ya 'kidemokrasia' yakandamiza wanachuo wanaopinga unyama wa Israel, 500 wakamatwa

Polisi wa Marekani wamewakamata zaidi ya waandamanaji 500 wakati wa msako mkali dhidi ya waandamanaji wanaounga mkono Palestina kwenye kampasi za vyuo vikuu kote nchini humo.

Polisi wa kupambana na ghasia walitumia viuwasho vya kemikali na gesi ya kutoa machozi dhidi ya waandamanaji walioweka kambi licha ya maonyo na vitisho vya polisi kutoka Massachusetts hadi California, wakipinga vita vya kinyama na mauaji ya kimbari yanayofanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Wapalestina katika Ukanda wa Ghaza.
 
Waandamanaji kadhaa walikamatwa katika vyuo kikiwemo Chuo Kikuu cha Jimbo la Ohio, Chuo Kikuu cha Minnesota, Chuo Kikuu cha Indiana na Chuo Kikuu cha Princeton.
 
Katika Chuo Kikuu cha Emory huko Atlanta, polisi walipambana na waandamanaji, ikiwa ni pamoja na wanafunzi kutoka vyuo vikuu vingine vya Atlanta na wanaharakati wa eneo hilo na kuwakamata waandamanaji kadhaa, ikiwa ni pamoja na washiriki wa kitivo.
Askari polisi wakimtia nguvuni mwanachuo mwanaharakati

Video zinasambazwa kwenye mitandao ya kijamii, zikionyesha maafisa wakitumia gesi ya kutoa machozi na pingu kuwatia nguvuni waandamanaji.

Kamatakamata za hivi karibuni zikifuatiwa na nyingine katika Chuo Kikuu cha Columbia, Yale, Brown na New York, imekuja wakati idadi zaidi ya wanachuo walijiunga na maandamano baada ya hatua iliyochukuliwa siku ya Jumatano iliyopita na Rais Joe Biden ya kuidhinisha dola bilioni 26 za msaada kwa Israel ili kuendeleza vita na mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina wa Ghaza.

Makundi ya wanachuo na wanaharakati katika kila pembe ya Marekani sasa yanautaka uongozi wa vyuo vikuu vyao kukata uhusiano wa kifedha kwa utawala wa Kizayuni wa Israel, ambao vita vyake vya kikatili kwenye Ukanda wa Ghaza vimeua zaidi ya watu 34,300 tangu mapema Oktoba.

Vuguvugu hilo la wanachuo wanaopinga Israel tayari limesambaa katika nchi nyingine za Magharibi ikiwemo Uingereza, Ufaransa na Australia.../

 

Tags