Waziri Mkuu Ufaransa: Kuna hatari Waislamu wakashambuliwa
Waziri Mkuu wa Ufaransa ametahadharisha kuhusu hatari ya kushambuliwa Waislamu nchini humo.
Manuel Valls ameliambia Bunge la Ufaransa kwamba kuna hatari Waislamu wakashambuliwa nchini humo na kwamba Ufaransa imo katika vita ngumu na ya muda mrefu.
Valls ameashiria mashambulizi ya kigaidi yaliyoilenga Ufaransa katika miezi ya hivi karibuni na kusema kuwa, nchi hiyo itaendelea kukabiliwa na mashambulizi kama hayo.
Waziri Mkuu wa Ufaransa amewataka wananchi wa nchi hiyo kuwa na umoja na mshikamano katika kupambana na ugaidi kwa sababu magaidi wanataka kuzusha hofu, woga na migawanyiko katika jamii kupitia mshambulizi hayo.
Waziri Mkuu wa Ufaransa amesisitiza udharura wa kulindwa raia wote wakiwemo Waislamu na utamaduni wa Kiislamu.
Wakati huo huo wabunge wa Ufaransa wamerefusha sheria ya hali ya hatari iliyoanza kutekelezwa nchini humo baada ya mashambulizi ya kigaidi ya Paris Novemba mwaka 2015.