Reuters: Trump amemwambia Zelensky anataka vita "visimamishwe mara moja"
https://parstoday.ir/sw/news/world-i120048-reuters_trump_amemwambia_zelensky_anataka_vita_visimamishwe_mara_moja
Rais mteule wa Marekani Donald Trump amemwambia Rais Vladimir Zelensky wa Ukraine na Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa kwamba anataka kukomeshwa uhasama wa vita kati ya Russia na Ukraine haraka iwezekanavyo. Hayo ni kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters likizinukuu duru kadhaa.
(last modified 2024-12-12T07:02:43+00:00 )
Dec 12, 2024 07:02 UTC
  • Reuters: Trump amemwambia Zelensky anataka vita

Rais mteule wa Marekani Donald Trump amemwambia Rais Vladimir Zelensky wa Ukraine na Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa kwamba anataka kukomeshwa uhasama wa vita kati ya Russia na Ukraine haraka iwezekanavyo. Hayo ni kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters likizinukuu duru kadhaa.

Watatu hao walikutana wiki iliyopita mjini Paris, ambapo walifanya mazungumzo kuhusu mzozo wa Ukraine, licha ya Trump kuripotiwa kuwa na hatihati ya kuhudhuria kikao hicho.
 
Kwa mujibu wa duru zilizonukuliwa na Reuters, baada ya mkutano huo, Trump alidai kwamba Ukraine "ingependa kufikia makubaliano" ya kumaliza mzozo na Russia. Zelensky, hata hivyo, alisisitiza kwamba Kiev lazima ipatiwe kwanza hakikisho madhubuti la usalama, akikataa pia kufikia makubaliano yoyote ya kuachia maeneo ya Ukraine yanayoshikiliwa na Russia.
 
Vyanzo vinne vimeitaarifu Reuters kwamba, katika mazungumzo yao yaliyochukua muda wa dakika 35, viongozi hao watatu "hawakujadili kwa undani maono yoyote ya kufikia amani," lakini Trump alisisitiza kwamba "anataka kusitishwa mapigano mara moja na kufanyika mazungumzo ili kumaliza vita haraka." 

Katika kipindi chote cha kampeni zake za kuwania urais, Trump aliahidi mara kadhaa kwamba angemaliza mzozo wa Ukraine ndani ya "saa 24" baada ya kuchukua madaraka, bila kutoa maelezo maalumu kuhusu namna atakavyofanikisha suala hilo.

Hata hivyo, inaaminika kuwa atatumia kitisho cha kupunguzwa misaada ya Marekani ili kumshurutisha kiongozi wa Ukraine Vladimir Zelensky kufanya mazungumzo, na tishio la kuongeza misaada hiyo kumshinikiza Rais wa Russia Vladimir Putin akubali kuketi kwenye meza ya mazungumzo.

Wakati wa majira ya kiangazi mwaka huu, Rais wa Russia alitangaza kuwa, Moscow itatangaza mara moja usitishaji vita na kuanza mazungumzo ya amani papo hapo mara tu Kiev itakapoondoa wanajeshi wake katika maeneo yote ya Russia, zikiwemo jamhuri za Donetsk na Lugansk, na mikoa ya Kherson na Zaporozhye.../