Moto wa Los Angeles; Ishara ya uzembe wa serikali ya Marekani
(last modified Sat, 11 Jan 2025 10:44:14 GMT )
Jan 11, 2025 10:44 UTC
  • Moto wa Los Angeles; Ishara ya uzembe wa serikali ya Marekani

Mji wa Los Angeles katika jimbo la California, Marekani, umekuwa ukiteketea kwa moto usiozuilika kwa siku kadhaa sasa katika msimu wa baridi kali na kuwaacha maelfu ya watu bila ya makazi. Moto huo pia umesababisha hasara na uharibifu mkubwa unaotajwa kuwa ni wa aina yake katika historia ya majanga nchini Marekani.

Rais Joe Biden wa Marekani siku ya Alhamisi alisema  kuwa moto wa mwituni ulioukumba mji wa Los Angeles ni mkubwa, haribifu na mbaya zaidi kuwahi kushuhudiwa katika historia ya California. 

Moto huo ambao haujawahi kushuhudiwa huko Los Angeles, ulianza siku ya Jumanne, Januari 7, na hadi sasa umeua watu 11 na kuwalazimisha wengine 200,000 kuhama na kukimbilia maeneo salama. Mabadiliko ya tabianchi, ukame na upepo mkali wa Santa Ana vimetajwa kuwa sababu ya moto huo. Viongozi wa Marekani na vyombo vya habari vya nchi hiyo vimedai kuwa hali ya hewa ndio chanzo cha moto huo. Wameeleza kuwa, sehemu kubwa ya eneo hilo inasumbuliwa na ukame mkubwa na kkwamba mimea mikavu ndio sababu ya kuibuka moto huo na kuenea  haraka. Katika upande mwingine,  upepo mkali wa  Santa Ana ulivuma kwa kasi ya maili 100 kwa saa  katika maeneo yenye mgandamizo wa chini kusini mwa California, na kusababisha uharibifu mkubwa.

Moto mkubwa wa aina yake waikumba Los Angeles 

Imetabiriwa kuwa moto huo utaendelea hadi wakati wa kunyesha mvua siku zijazo. Maelfu ya watu wamebaki bila ya makazi huku moshi mzito ukiwalazimisha maafisa wa serikali ya Marekani kutangaza dharura ya afya ya umma. Moto wa Los Angeles umeharibu majengo 12,300, idadi ya watu waliopoteza maisha na majengo yaliyoharibiwa  ikitazamiwa kuongezeka. Robert Lona,  Sherifu wa Kaunti ya Los Angeles alisema jana Ijumaa kwamba, wakaazi 166,800 wa mji huo wataamrishwa kuhama. Ameongeza kuwa, nyumba 57,830 pia ziko katika hatari ya kuathiriwa na moto. 

Hasara na madhara yaliyosababishwa na moto huo yanakadiriwa kuwa dola bilioni 135 hadi 150. Rais Joe Biden wa Marekani ameutaja moto wa Los Angeles kuwa ni maafa makubwa. Makamu wa Rais wa nchi hiyo, Kamala Harris pia ameutaja moto huo wa mwituni kuwa ni "mwisho wa dunia" na kukosoa kitendo cha mashirika ya bima ya Marekani cha kufutia bima za familia zilizoathiriwa na moto.

Moto haribifu ulioitafuna Los Angeles 

Pamoja na kusambaa moto katika jimbo la California na kusababisha hali iliyotajwa na wengi kuwa ni maafa, kushindwa utawala wa Biden kushughulikia hali hiyo ya maafa pia kumemulikwa pakubwa. Moto huo mkubwa umepelekea kukosolewa pakubwa serikali ya Biden na kushindwa taasisi za Marekani kulipatia ufumbuzi suala hilo. Serikali ya Biden  ilipunguza bajeti ya Idara ya Zimamoto ya Los Angeles hadi dola milioni 17.6 kuanzia mwaka jana hadi mwaka huu wa 2025 licha ya matukio makubwa ya moto yanayolikumba jimbo la California. Kiwango hiki ni cha pili kwa ukubwa miongoni mwa mapunguzo mengine ya bajeti  za kuendeshea miji. 

Gazeti la New York Times limeandika kuwa uamuzi huo wa Biden umeisababishia hali ngumu Idara ya Zimamoto ya Los Angeles na hivyo kushindwa kukabiliana na "jahanamu" hiyo. Hii ni katika hali ambayo vifaa vya  maji ya kuzimia moto viko tupu na wafanyakazi wa zimamoto wamekwamishwa pakubwa kutokana vifaa hivyo kuishiwa maji.  

Donald Trump, Rais mteule wa Marekani, ni kati ya watu walioikosoa serikali ya  joe Biden, na watu wake wa karibu akiwemo mwanawe, Donald Trump Jr, ambao wamekosoa vikali utendaji usiofaa, mapungufu na upuuzaji wa serikali ya Biden katika kushughulikia janga hilo la moto. 

Donald Trump amemtusi Gavana wa California, Gavin Newsom kwenye mtandao wa kijamii wa "X" na kubadilisha sehemu ya jina lake la mwisho kuwa "takataka". Ameandika: "Moja ya sehemu bora na maridadi zaidi za Marekani inateketea kwa moto. Majivu yameenea kila mahali, na 'takataka mpya Gavin' anapasa kujiuzulu. Yeye ndiye mwenye makosa. Baya zaidi ni kuwa hakuna  maji kwa ajili ya mabomba ya kuzimia moto wala ndege. Hili ni janga halisi." 

Wakati huo huo mwana wa kiume wa Trump yaani Donald Trump Junior, ameuhusisha moto wa California na msaada wa Marekani kwa Ukraine na kumtaja Biden kuwa anabeba dhima katika uwanja huo. Mtoto huyo wa Trump amechapisha vichwa vya habari kwenye mitandao ya kijamii ambavyo vinaonyesha namna Idara ya Zimamoto ya Los Angeles huko nyuma ilivyotoa vifaa vyake ili kuisaidia Ukraine. 

Nukta muhimu ni kuwa usimamizi mbaya wa Serikali ya Shirikisho ya Marekani katika kushughulikia majanga ya kimaumbile kama vile Kimbunga cha Katrina kilichoikumba nchi hiyo mwaka 2005 katika majimbo kadhaa ya kusini mwa nchi, na vilevile moto wa miaka iliyopita huko California na serikali kushindwa kuwasaidia waathiriwa wa maafa hayo ni moja ya masuala ambayo yamedhihirika wazi zaidi. Wakati huo huo serikali hii ya Marekani, ambayo haiwezi kukabiliana na migogoro na matatizo yake ya ndani, inadai kushughulikia na kuipatia ufumbuzi migogoro ya kikanda na kimataifa.