Kugonga mwamba mpango wa Serikali ya Marekani wa kuiwekea vikwazo ICC
(last modified Fri, 31 Jan 2025 02:49:20 GMT )
Jan 31, 2025 02:49 UTC
  • Kugonga mwamba mpango wa Serikali ya Marekani wa kuiwekea vikwazo ICC

Baraza la Seneti la Marekani halijauidhinisha mswada wa vikwazo dhidi ya Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC, vikwazo ambavyo ni jibu la utoaji vitisho linalolenga kuiadhibu mahakama hiyo kwa uamuzi wake wa kutoa hati za kukamatwa waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu na aliyekuwa waziri wa vita wa utawala huo wa Kizayuni Yoav Gallant.

Kongresi ya Marekani

Siku ya Jumanne, Januari 28, mswada huo ambao ulikuwa umeshapitishwa na Baraza la Wawakilishi la Marekani, ulipigiwa kura katika Baraza la Seneti, na matokeo yakawa ni kuungwa mkono kwa kura 54 na kupingwa kwa kura 45. Ili mswada huo upite ulihitaji kura 60 za wajumbe wa Baraza la Seneti la Marekani, ambalo lina jumla ya Maseneta 100. Upigaji kura wa kupitisha mswada huo wa vikwazo dhidi ya ICC ulitawaliwa zaidi na mielekeo ya kichama, ambapo karibu maseneta wote wa Democrat na wale wa kujitegemea waliupigia kura za kuupinga.

Mswada huo unaojulikana kama "Sheria ya Kukabiliana na Mahakama isiyo ya Kisheria" ya ICC unalenga kuiwekea vikwazo Mahakama ya Kimataifa ya Jinai kwa sababu ya kuamua kumchunguza, kumweka kizuizini au kumshtaki raia yeyote wa Marekani au wa washirika wake, ikiwa ni pamoja na Israel, ambayo si mwanachama wa mahakama hiyo. Wademokrati katika Baraza la Seneti wametangaza kuwa japokuwa wanakubaliana na sehemu kubwa ya mswada huo, lakini una sura ya kiujumla sana na kuna hofu ya kuwekewa vikwazo wafanyakazi wa ngazi za chini wa Mahakama ya ICC na kuzuka mpasuko pia kati ya Marekani na waitifaki wake wakuu.

Chuck Schumer, kiongozi wa Wademokrati katika Seneti aliituhumu Mahakama ya Kimataifa ya Jinai kwamba ina "mielekeo dhidi ya Israel"; lakini pamoja na hayo akawataka Wademokrati wenzake wapige kura za kuupinga mswada huo. Schumer alisisitiza kuwa mswada huo una nukta dhaifu nyingi sana, kiasi cha kuweza kupelekea kuwekewa vikwazo hata makampuni ya Marekani, yakiwemo mashirika yanayoisaidia ICC kujilinda na hujuma za wadukuzi wa nje.

Mswada wa kuiwekea vikwazo Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ulipitishwa katika Baraza la Wawakilishi la Marekani mnamo Alkhamisi, Januari 9, kwa kura 243 za 'ndiyo' dhidi ya 140 za 'hapana', ambapo Wademokrati 45 waliungana na Waripablikani kuunga mkono mswada huo.

Alkhamisi, Novemba 21, 2024, Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ilitoa hati za kukamatwa Netanyahu na Gallant kwa tuhuma za kufanya jinai za kivita, jinai dhidi ya binadamu, na kutumia njaa kama silaha kwa kuwatesa kwa njaa Wapalestina wa Ghaza. Uamuzi huo wa ICC ambao ni wa kihistoria, uliukasirisha mno utawala wa Kizayuni hasa kwa vile kwa muda wote kabla ya hapo na kwa uungaji mkono wa Marekani, utawala huo ulikuwa ukijaribu kuyaonyesha makundi ya Muqawama ya Palestina hususan Hamas kuwa ni kundi la kigaidi na mfanyajinai; na mkabala wake, kujionyesha wenyewe kuwa ni mhanga na muathiriwa wa jinai za kundi hilo. Hata hivyo, jinai ambazo hazijawahi kushuhudiwa mfano na ukubwa wake, ambazo Israel imewafanyia Wapalestina madhulumu wa Ghaza, mauaji ya makusudi ya kimbari uliyofanya dhidi ya watu hao, kutumia silaha ya kuwatesa kwa njaa, kuwazuilia misaada na hata kulipiga marufuku Shirika la Umoja wa Mataifa la Kushughulikia Wakimbizi Wapalestina UNRWA, yote hayo yameibua wimbi kubwa kimataifa la kuulaani utawala huo haramu na kutaka viongozi wake wakuu wafuatiliwe na kupandishwa kizimbani na Mahakama ya Kimataifa ya Jinai; ambapo hatimaye mnamo mwezi Mei 2024, Karim Khan, Mwendesha Mashtaka Mkuu wa ICC, aliwaomba majaji wa mahakama hiyo ya kimataifa ya jinai watoe hati ya kukamatwa Netanyahu na Gallant, ombi ambalo lilikubaliwa.

Kutoka kushoto: Netanyahu, Karim Khan na Gallant

Utawala wa Kizayuni na Marekani, ambayo ndiyo muungaji mkono mkuu wa utawala huo, zilishtushwa na kushangazwa na hatua hiyo ya ICC na hivyo zikatoa mijibizo mikali dhidi ya mahakama hiyo. Ijapokuwa jinai za utawala wa Kizayuni, hususan mauaji ya kimbari ya watu wa Ghaza na utumiaji wa silaha ya njaa dhidi ya watu wa eneo hilo ni jambo lililo wazi kabisa na lisiloweza kukanushika, lakini Marekani imetumia njia na mbinu kadhaa ili kuzuia uchunguzi wa jinai za utawala huo uliofanywa na taasisi za kimataifa za kimahakama kama Mahakama ya Kimataifa ya Haki ICJ na Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC. Baada ya Afrika Kusini kuwasilisha mashtaka dhidi ya Israel kwenye Mahakama ya Kimataifa ya Haki kwa kukiuka Mkataba wa Geneva wa mwaka 1948 wa Kuzuia Mauaji ya Kimbari, Ikulu ya White House ilitangaza waziwazi upinzani wake dhidi ya hatua hiyo. Kuhusiana na kutolewa hati za kukamatwa Netanyahu na Gallant, maafisa waandamizi wa Marekani walitoa tamko kali pia la kupinga uamuzi huo. Katika mjibizo aliotoa dhidi ya uamuzi huo, rais wa wakati huo wa Marekani Joe Biden alidai uamuzi huo eti ni wa "kuaibisha". Seneta mwenye misimamo mikali na ya kufurutu mpaka Lindsey Graham, yeye alifika hadi ya kutoa vitisho dhidi ya washirika wa Washington vya kuwawekea vikwazo iwapo watatekeleza agizo la Mahakama ya Kimataifa ya Jinai la kukamatwa Netanyahu na Gallant.

Hatua za waungaji mkono wa utawala wa Kizayuni wa Israel katika Bunge la Marekani la Kongresi za kuwasilisha mswada wa kuiwekea vikwazo Mahakama ya Kimataifa ya Jinai zimechukuliwa katika mwelekeo huo, yaani kutekeleza kitisho cha kuiwekea vikwazo mahakama hiyo. Hata hivyo, licha ya mswada huo kupitishwa katika Baraza la Wawakilishi, upinzani wa Maseneta wa Democrat na wa kujitegemea katika Baraza la Seneti, ambao umekwamisha upitishaji wake, umeifunga mikono Marekani na kuifanya ishindwe kutekeleza kitisho chake hicho cha kuiwekea vikwazo ICC…/