Mwanasiasa mwenye chuki dhidi ya Uislamu Denmark avunjia heshima Qur'ani
Mwanasiasa mwenye uraia pacha wa Sweden na Denmark na mwenye chuki dhidi ya Uislamu, Rasmus Paludan kwa mara nyingine tena ameivunjia heshima Qur'ani Tukufu kwa kuchoma moto nakala ya kitabu hicho kitakatifu cha Waislamu katika mji mkuu wa Denmark, Copenhagen.
Paludan, mwenye umri wa miaka 43, mwasisi na kiongozi wa chama kinachopinga uhamiaji cha Stram Kurs, kwa mara nyingine tena ameughadhabisha umma wa Kiislamu kwa kufanya kitendo hicho cha kufuru nje ya ubalozi wa Uturuki nchini Denmark.
Video iliyosambazaa kwenye mitandao ya kijamii inamuonyesha Paludan akiivunjia heshima Qur'ani Tukufu, kitendo kinachokera sana Waislamu duniani kote. Uafriti huu mpya umefanyika katika hali ambayo, Mahakama ya Denmark mnamo Agosti mwaka 2023 iliamua kupiga marufuku vitendo vya kuvunjiwa heshima Qur'ani Tukufu kufuatia taathira mbaya za hatua hizo.
Hatua ya mwanasiasa huyo mwenye misimamo ya kufurutu ada ya kuvunjia heshima Qur'ani Tukufu nchini Denmark inajiri siku chache baada ya mkimbizi wa Iraq, Salwan Momika aliyekuwa na tabia kama hiyo, kuangamizwa kwa kupigwa risasi akiwa nyumbani kwake katika mji wa Sodertalje, Sweden mnamo Januari 30.

Vitendo vichafu vya mara kwa mara vya Momika wa kunajisi na kuvunjia heshima nakala za Qur'ani Tukufu nchini Sweden vimekuwa wakiwakasirisha Waislamu na hata wasiokuwa Waislamu kote ulimwenguni.
Katika miaka ya hivi karibuni, Denmark na Sweden zimegeuka kuwa chaka la maadui wa Uislamu ambao wamekuwa wakiendesha kampeni kubwa za chuki dhidi ya Uislamu na Waislamu.