Rais wa Mexico ampokea rasmi balozi mpya wa Palestina
Rais wa Mexico, Claudia Sheinbaum amepokea rasmi hati za utambulisho za Balozi wa Palestina Nadya R. H. Rasheed katika Ikulu ya Mexico City.
Wote wawili walipiga picha ambayo imetumwa kwenye akaunti ya ubalozi wa Palestina ya mtandao wa X, ikiwa na ujumbe wa shukrani za Rasheed, ambaye amesifu na kupongeza msimamo wa Mexico juu ya vita vya Israel dhidi ya Gaza.
"Ni heshima na fursa iliyoje kukutana na kiongozi ambaye anawakilisha kiini cha kweli cha ubinadamu - anayetetea haki za binadamu kwa wote, bila kujali dini au turathi, kama ambavyo ulimwengu unapaswa kujitahidi kufanya," ameandika.
Sheinbaum, rais wa kwanza mwanamke wa Mexico ambaye ni Myahudi, ametoa wito wa kutambuliwa kwa taifa huru la Palestina. Mwezi Oktoba mwaka jana, kiongozi huyo wa Mexico alilaani vikali "uchokozi dhidi ya watu wa Palestina."
Upokeaji wa hati za utambulisho wa Balozi wa Palestina unafanyika sanjari na kuendelea mashambulizi mapya ya Israel huko Gaza, ambayo yamesababisha mauaji ya Wapalestina 700, karibu nusu yao wakiwa watoto, katika siku chache zilizopita.
Rais wa zamani wa Mexico, Andrés Manuel López Obrador alilitambua rasmi taifa la Palestina mnamo Juni 2023, na kuupandisha uwakilishi wa Palestina nchini Mexico kutoka kwa ujumbe maalum hadi hadhi kamili ya ubalozi.