Amnesty International: Magharibi ndiyo inayobeba dhima ya machafuko duniani
(last modified Tue, 16 Feb 2016 01:09:07 GMT )
Feb 16, 2016 01:09 UTC
  • Amnesty International: Magharibi ndiyo inayobeba dhima ya machafuko duniani

Shirika la Msamaha Duniani limesisitiza kuwa, uvunjaji mkubwa wa haki za binadamu unaotokea katika kona mbalimbali za dunia unafanyika kwa msaada wa silaha za nchi za Magharibi na kwamba Magharibi ndiyo inayopaswa kubeba ya dhima ya machafuko yote hayo.

Salil Shetty, Katibu Mkuu wa Shirika la Msamaha la Amnesty International amesema hayo kwenye mkutano wa amani wa mjini Munich, Ujerumani na kuongeza kuwa, nchi za Magharibi ni moja ya wabeba dhima wakuu wa mapigano na machafuko yanayotokea katika kona mbalimbali za dunia.

Amesisitiza kuwa, sehemu kubwa ya vitendo vya uvunjaji wa haki za binadamu vinavyotokea duniani leo vinafanywa kwa kutumia silaha ambazo madola ya Magharibi yanawapa wanaotenda jinai hizo.

Ameongeza kuwa, jambo la kusikitisha zaidi ni kuona kuwa baadhi ya magenge hayo yanayofanya jinai yamepewa mafunzo na majeshi ya nchi za Magharibi.

Katibu Mkuu wa Shirika la Msamaha Duniani amesema kuwa, dunia hivi sasa imekumbwa na mgogoro wa ukosefu wa usalama na wimbi la wakimbizi na kwamba ni wajibu kwa jamii ya kimataifa kuwalinda raia na watu wasio na ulinzi.

Amesema, zaidi ya asilimia 90 ya wakimbizi hukimbilia nchi jirani na hawatii mguu wao katika nchi za Magharibi (licha ya nchi hizo za Magharibi kuwa wachangiaji wakuu wa jinai zinazotendeka duniani leo).