Marekani na Uingereza; madai ya uongo kuhusu haki za binadamu
https://parstoday.ir/sw/news/world-i133062-marekani_na_uingereza_madai_ya_uongo_kuhusu_haki_za_binadamu
Ripoti kuhusu ukiukaji wa haki za binadamu nchini Marekani na Uingereza zimechapishwa na Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Iran.
(last modified 2025-11-12T06:10:22+00:00 )
Nov 12, 2025 02:31 UTC
  • Marekani na Uingereza; madai ya uongo kuhusu haki za binadamu

Ripoti kuhusu ukiukaji wa haki za binadamu nchini Marekani na Uingereza zimechapishwa na Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Iran.

Jumapili ya tarehe 9 Novemba Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilichapishwa ripoti ya kila mwaka kuhusu hali ya haki za binadamu nchini Marekani na Uingereza kuanzia Septemba 2024 hadi Septemba 2025.

Ripoti hiyo ina sehemu mbili: "Ukiukaji wa haki za binadamu katika ngazi ya kitaifa" na "Ukiukaji wa haki za binadamu katika viwango vya juu na kimataifa."

Katika ripoti hiyo kuhusu Marekani, katika sehemu ya kwanza inayohusu ukiukwaji wa haki za binadamu katika ngazi ya kitaifa, kuna sura 8 ambazo zina ukiukwaji mwingi wa haki za binadamu, kama vile ukiukwaji wa haki ya kuishi, uhuru na usalama wa mtu binafsi, ukiukwaji wa haki za wafungwa, ukiukwaji wa uhuru wa kujieleza na kukusanyika kwa amani, ubaguzi wa kimuundo, ukiukwaji wa haki za wahamiaji na wakimbizi, ukiukwaji wa haki za wanawake, ukosefu wa usawa na ugavi usio wa haki wa mali.

Sehemu ya ukiukaji wa haki za binadamu katika ngazi za kimataifa pia imechapishwa katika sura nne, ambazo ni pamoja na kuunga mkono utawala wa Kizayuni katika mauaji ya halaiki ya Gaza, operesheni za kijeshi za kuvuka mpaka na mauaji ya raia, hatua za kulazimisha upande mmoja, na kujiondoa katika mashirika ya kimataifa.

Sura mojawapo ya ripoti ya haki za binadamu nchini Marekani inazungumzia shambulizi dhidi ya vituo vya nyuklia vya Iran, na vilevile ushirikiano wa Marekani na utawala haramu wa Israel katika uvamizi wake wa kijeshi dhidi ya Iran.

Maandamano ya wanachuo Marekani ya kuunga mkono Palestina

 

Licha ya kauli mbiu zinazotolewa na serikali ya Marekani kuhusu kuheshimu haki za binadamu na ulinzi wa haki za mtu binafsi na za kijamii na uhuru na haki za kiraia katika nchi hiyo, utendaji wa serikali ya Washington katika masuala mbalimbali kama vile kukabiliana na watu wa asili, walio wachache na Wamarekani wenye asili ya Afrika, hali ya wafungwa, uvamizi wa faragha na kesi nyingine nyingi zinaonyesha madai ya uongo ya Washington kuhusu kutetea haki za binadamu. Ukiukaji wa haki za binadamu nchini Marekani hufanyika katika nyanja na engo mbalimbali.

Marekani inahesabiwa kuwa mojawapo ya wakiukaji wakubwa wa haki za watu wa asili na walio wachache. Lakini kesi ya wazi zaidi na ya muda mrefu ya ukiukaji wa haki za binadamu nchini humo inahusiana na ubaguzi wa rangi na kijinsia. Ubaguzi wa rangi nchini Marekani, hasa dhidi ya Wamarekani wenye asili ya Afrika, kwa muda mrefu sasa limekuwa suala la kawaida kabisa.

Ukweli wa mambo ni kuwa historia ya Marekani inaonyesha kwamba ubaguzi wa rangi katika nchi hiyo unafungamana na historia yake. Ukiukaji mwingine wa haki za binadamu nchini Marekani unahusiana na jamii kwa ujumla, ikiwa ni pamoja na kuongezeka kwa matukio ya uhalifu wa kikatili na kuenea kwa matumizi ya silaha za moto, jambo ambalo limezua tishio kubwa kwa usalama wa mtu binafsi na jamii kwa ujumla.

Kwa hivyo, haki ya usalama, ambayo inachukuliwa kuwa moja ya haki za msingi zaidi za kibinadamu, inakiukwa mara kwa mara nchini Marekani. Ukiukaji mwingine muhimu wa haki za binadamu nchini Marekani ni ukosefu wa uhuru wa kujieleza na kufunguliwa mashtaka watu kwa kosa la kufichua ukiukaji wa faragha na ujasusi dhidi ya raia unaofanywa na serikali.

Kadhalika, hali mbaya ya jela za Marekani na idadi kubwa ya wafungwa katika nchi hiyo imepelekea mashirika ya kutetea haki za binadamu kutembelea baadhi ya jela hizo na kuandaa ripoti zinazoashiria hali ya kinyama ya wafungwa hao.

Jela ya Guantanamo Bay

 

Kwa upande wa nje ya nchi, Marekani imefanya ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu tangu kuanzishwa kwake, na mashambulizi makubwa nje ya mipaka yake na mauaji ya raia. Jinai za Marekani katika nchi za Vietnam, Iraq, Afghanistan, Syria na Yemen, na kushirikiana kwake na Israel katika mauaji ya halaiki ya Wapalestina katika Ukanda wa Gaza, ambayo yalisababisha vifo vya mamia ya maelfu ya watu wasio na hatia, ni miongoni mwa visa muhimu zaidi vya ukiukwaji wa haki za binadamu unaofanywa na serikali ya Marekani.

Ukatili wa haki za binadamu uliofanywa katika jela za Abu Ghuraib na Bagram, pamoja na kile kinachoitwa mashambulizi ya kupambana na ugaidi kwa kutumia ndege zisizo na rubani, ni miongoni mwa ukiukwaji wa wazi wa haki za binadamu unaofanywa na Marekani nje ya nchi.

Ukiukaji mwingine wa haki za binadamu nje ya Marekani ni pamoja na kuwekwa kizuizini kwa muda usiojulikana wafungwa bila kufunguliwa mashtaka katika Ghuba ya Guantanamo na matumizi ya aina mbalimbali za mateso dhidi yao, jambo ambalo limesababisha maandamano mengi dhidi ya nchi hiyo yanayofanywa na mashirika ya ndani na kimataifa ya kutetea haki za binadamu.

Uingereza ambayo ni mshirika wa kimkakati wa Marekani, pia ina historia mbaya ya ukiukaji wa haki za binadamu, hasa wakati wa ukoloni, na inaendelea kukiuka haki za binadamu. Katika suala hili, katika ripoti ya ukiukwaji wa haki za binadamu nchini Uingereza, katika sehemu ya kwanza, inayohusu ukiukwaji wa haki za binadamu katika ngazi ya kitaifa, kumetajwa matukio 12 ambayo ni pamoja na ukiukwaji wa haki ya kuishi, ukiukwaji wa uhuru wa kukusanyika kwa amani, ukiukwaji wa haki za wahamiaji na wakimbizi, kukatwa huduma za umma, ukatili wa polisi dhidi ya wanawake na raia wenye asili ya Afrika, ubaguzi wa rangi na mbari, ukiukwaji wa haki ya afya, ukiukwaji wa uhuru wa kujieleza, kutumia vibaya akili mnemba, ukatili dhidi ya haki za wanawake na wasichana, unyanyasaji wa haki za watoto na mazingira mabaya katika magereza.

Sehemu ya pili ya ripoti ya Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Iran kuhusu ukiukaji wa haki za binadamu nchini Uingereza inahusiana na ukiukwaji wa haki za binadamu kimataifa, na nje ya mipaka unaofanywa na serikali ya London ambayo kama ilivyo Washington imekuwa mstari wa mbele kujinadi kuwa mtetezi wa haki za binadamu. Katika sehemu hii kumezungumziwa maudhui mbili: Ukiukwaji wa haki za binadamu katika uwanja wa biashara, ikiwa ni pamoja na usafirishaji wa bidhaa hatari na taka, usafirishaji wa viuatilifu vilivyopigwa marufuku, na kufikia haki na ushiriki wake katika mauaji ya kimbari huko Gaza.