Trump aamua kutozungumzia hali ya afya ya Hillary Clinton
Mgombea uraia kwa tiketi ya chama cha Republican nchini Marekani, Donald Trump, amenyamanzia kimya kuzungumzia hali ya afya ya mshindani wake wa chama cha Democrat, Hillary Clinton.
Trump ameamua kutozungumzia suala la hasimu wake Clinton kupatwa na maradhi ya Homa ya Mapafu. Kwa mujibu wa ripoti hiyo, tayari mgombea huyo wa chama cha Republican ameitaka timu yake ya kampeni kutosambaza kwenye mitandao ya kijamii habari yoyote kuzungumzia afya ya Hillary Clinton.
Jumapili ya jana timu ya kampeni ya Bi Hillary iliamua kuweka wazi katika tukio la kuwakumbuka wahanga wa shambulio la Septemba 11 nchini Marekani juu ya maradhi hayo ikiwa ni baada ya kupita siku mbili tangu alipoambukizwa. Kufuatia hali hiyo Clinton ameamua kufuta safari za jimbo la California leo na kesho Jumanne. Daktari wa Hillary Clinton, Lisa Bardack amesema kuwa mteja wake alipatwa na ugonjwa huo wa homa ya mapafu tokea Ijumaa na kwamba alipatwa na homa na kuishiwa na maji mwilini jana Jumapili katika kumbukumbu za Septemba 11.
Baada ya hali hiyo, Clinton alilazimika kuondoka mapema eneo la tukio, ambapo picha zilimuonyesha akisaidiwa na msaidizi wake, huku akitaka kuanguka alipokaribia kwenye gari. Hii ni katika hali ambayo katika siku za hivi karibuni Donald Trump alizungumza kuhusu kuwa na na matatizo makubwa ya kiafya ya hasimu wake huyo, na hivyo kuchochea uvumi na tetesi mbalimbali katika mitandao ya kijamii.