Rais Park Geun-hye: Vitisho vya Korea Kaskazini vinatia wasiwasi
https://parstoday.ir/sw/news/world-i16003-rais_park_geun_hye_vitisho_vya_korea_kaskazini_vinatia_wasiwasi
Rais Park Geun-hye wa Korea Kusini amesema kuwa, vitisho vya nchi jirani ya Korea Kaskazini ni halisi na vinatia wasiwasi mkubwa.
(last modified 2026-02-03T09:36:48+00:00 )
Sep 25, 2016 04:16 UTC
  • Rais Park Geun-hye: Vitisho vya Korea Kaskazini vinatia wasiwasi

Rais Park Geun-hye wa Korea Kusini amesema kuwa, vitisho vya nchi jirani ya Korea Kaskazini ni halisi na vinatia wasiwasi mkubwa.

Rais Park Geun-hye ameyasema hayo katika kikao maalumu cha kuchunguza masuala ya usalama na uchumi na changamoto za Korea Kaskazini kilichofanyika mjini Seoul. Kikao hicho cha kwanza kufanyika tangu mwaka 2013 kimehudhuriwa pia na viongozi 100 wa ngazi ya juu akiwemo Waziri Mkuu, Hwang Kyo-ahn, Waziri wa Mambo ya Nje, Yun Byung-se na Waziri wa Ulinzi Han Min-goo. 

Kim Jong-un, Kiongozi wa Korea Kaskazini

Rais Park Geun-hye wa Korea Kusini amesema kuwa, vitisho vya Korea Kaskazini ni vya kweli na kwa ajili hiyo nchi yake inatakiwa kuchukua hatua za maana kukabiliana navyo. Kwa mujibu wa duru za habari nchini humo, Korea Kusini imeazimia kutumia njia za kisasa  kwa ajili ya kukabiliana na changamoto za usalama na kiuchumi.

Sehemu ya majaribio ya makombora ya Korea Kaskazini

Kadhalika katika kikao hicho viongozi wa serikali ya Seoul walijadili kwa kina njia za kukabiliana na vitisho vya Korea Kaskazini sanjari na kuzuia ongezeko la harakati za nyuklia za Pyongyang. Mwishoni mwa kikao hicho imetangazwa kuwa, vitisho na majaribio ya makombora na nyuklia ya Korea Kaskazini katika mpaka wa nchi hiyo, vimefikia kiwango cha hatari na kwamba ni lazima kukabiliana na hali hiyo.