Wamarekani wahofia kutokea mashambulizi ya kigaidi wakati wa uchaguzi
-
Greg Abbott, Mkuu wa jimbo la Texas la Marekani
Viongozi wa serikali ya Marekani wameonya juu ya uwezekano wa kutokea mashambulizi ya kigaidi siku ya uchaguzi wa rais na kuwataka wananchi wajiandae kwa hilo.
Shirika la habari la Reuters limemnukuu Greg Abbott, Mkuu wa jimbo la Texas la Marekani akisema leo kuwa, kuna uwezekano magaidi wakafanya mashambulizi nchini humo wakati wa uchaguzi wa rais.
Mkuu huyo wa jimbo la Texas aidha amewataka wananchi wa Marekani kuwa macho kikamilifu na kama wataona kitu chochote kisicho cha kaawaida katika siku zijazo, waripoti haraka kwa maafisa usalama.
Tahadhari hiyo ya Greg Abbot imetolewa baada ya jeshi la polisi la FBI la Marekani kutangaza kuwa, kuna uwezekano wa kutokea vitisho vya usalama wakati wa kupiga kura kutoka kwa kundi la kigaidi la al Qaida nchini Marekani.
Majimbo ambayo kuna uwezekano mkubwa wa kutokea mashambulizi ya kigaidi kwa mujibu wa ripoti hiyo ni Texas, Virginia na New York.
Kabla ya hapo pia wanamgambo wanaoumuunga mkono mgombea urais kwa tiketi ya chama cha Republican nchini Marekani, Donald Trump, wanaojulikana kwa jina la Three Percent Security Force walikuwa wametishia kuwa wataanzisha ghasia na machafuko nchini humo iwapo mgombea huyo atashindwa katika uchaguzi ujao.
Kundi la wanamgambo la Three Percent Security Force linaloongozwa na afisa wa zamani wa Jeshi la Majini la Marekani, Chris Hill, linaunga mkono sera kuu za Donald Trump hususan suala la kuwafukuza wahajiri nchini Marekani, kuwazuia Waislamu wasiingie nchini humo na kujenga ukuta unaotenganisha Marekani na nchi ya Mexico.