Saudi Arabia inaunga mkono ugaidi barani Afrika
Gazeti la Washington Post la Marekani limeandika makala kuhusu kuenea Uwahhabi nchini Nigeria na kuongeza kuwa, utawala wa Saudi Arabia unaaunga mkono viongozi wa Mawahhabi ili waweze kueneza Uwahhabi nchini humo na kote barani Afrika.
Hakuna shaka kuwa, Saudi Arabia ina nafasi kubwa katika kueneza ugaidi wa Kiwahhabi kaskazini mwa Nigeria. Abubakar Gumi mmoja wa majaji wa ngazi za juu Nigeria na ambaye ana misimamo ya Kiwahhabi, mnamo mwaka 1978 alianzisha harakati ya Kisalafi ya Izala ambayo ina uhusiano wa karibu na Saudi Arabia. Hakuna shaka kuwa harakati za Kiwahhabi Nigeria zina uhusiano wa karibu na Saudi Arabia. Kundi la kigaidi la Boko Haram linaendeshwa kwa misingi ya itikaadi za ukufurishaji za Kiwahhabi na lina uhusiano wa karibu na Saudia. Wafuasi wa Boko Haram nchini Nigeria wamepata mafunzo ya itikadi za Kiwahhabi na hata mwanzilishi wa kundi hilo la kigaidi, Mohammad Yusuf ana uhusiano wa karibu na Saudi Arabia na aliwahi kuishi katika ufalme huo.
Saudi Arabia ni muungaji mkono mkubwa zaidi na mlezi wa fikra za kigaidi duniani. Kwa kuangazia harakati za ndani na nje ya Saudia, inabainika wazi kuwa aghalabu ya magaidi katika eneo la Magharibi mwa Asia na dunia nzima wana asili ya Saudi Arabia au wamevutiwa na fikra za Kiwahabi ambazo chimbuko lake ni Saudia. Aidha aghalabu ya magaidi wakufurishaji duniani wanapata himaya ya kifedha na kisilaha kutoka Saudi Arabia.
Mitandao ya magaidi wakufurishaji duniani inafuata itikadi bandia na isiyo ya kimantiki ya Uwahhabi. Itikadi hii potofu imekuwa na nafasi muhimu katika harakati za kigaidi za Saudia katika eneo na dunia nzima.
Kati ya malengo ya Saudia katika kuunda na kuunga mkono makundi ya kigaidi katika eneo ni kukabiliana na harakati za muqawama au mapambano ya Kiislamu ambazo zinazidi kupata nguvu katika eneo. Ili kupunguza ushawishi wa harakati hizo, Saudia inaeneza Uwahhabi katika jamii za Kiislamu.
Kuibua wimbi la kuogofya na kuhimiza malumbano ya kikaumu, kidini na kimadhehebu katika nchi za Kiislamu na maeneo mengine duniani ni lengo jingine la kuunda makundi ya magaidi wa Kiwahhabi.
Magaidi hao wenye misimamo mikali wanachochea vita katika nchi za Kiislamu kwa kuwakufurisha Waislamu wote wasiokubaliana na itikadi zao batili.
Hata waitifaki wa Saudi Arabia wamekiri mara kadhaa kuwa ufalme huo unahusika na makundi ya kigaidi. Kwa mujibu wa nyaraka zilizofichuliwa na mtandao wa WikiLeaks, Hilary Clinton, Waziri wa Zamani wa Mambo ya Nje Marekani, ambaye sasa anagombea urais wa nchi hiyo, amekiri kuwa, Saudi Arabia ni muungaji mkono mkubwa zaidi wa kifedha wa makundi ya kigaidi duniani.

Hillary Clinton pia amewahi kukiri hadharini kuwa, Marekani ikishirikiana na Saudia ilianzisha kundi la kigaidi la Al Qaeda. Clinton pia amekiri kuwa, Al Qaeda, Taliban, Lashkar Taiba ya Pakisan ni kati ya makundi ya kigaidi yanayopata uungaji mkono wa kifedha na kisilaha kutoka Saudi Arabia.
Hakuna shaka kuwa, uungaji mkono wa madola yanayopinga mwamko katika eneo ndio chanzo cha kuenea ugaidi. Ni wazi kuwa makundi ya kigaidi hayawezi kuwa na harakati pana Mashariki ya Kati na Afrika kama si uungaji mkono kutoka kwa madola kama hayo.
Makundi ya kigaidi yanayopata himaya ya Saudia kama vile ISIS au Daesh, Al Qaeda yana matawi yao kama vile Ansari Sharia ya kaskazini na magharibi mwa Afrika, Boko Haram ya Magharibi mwa Afrika, Al Shabab ya Afrika Mashariki n.k. na makundi mengine ya kigaidi barani Asia na hata Ulaya ni hatari kubwa kwa usalama wa dunia.