Zarif: Msaada wa kibinadamu kwa Yemen na Syria, jambo la dharura
Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema msaada wa kibinadamu kwa ajili ya watu wa Yemen na Syria ni jambo la dharura.
Mohammad Javad Zarif ameyasema hayo katika mazungumzo yake na Rais wa Slovakia Andrej Kiska mjini Bratislava na kuongeza kuwa, jambo kubwa wanalohitajia watu wa Yemen na Syria kwa sasa ni misaada ya kibinadamu.
Zarif amesema kuwa: "Kama mkuu wa Umoja wa Ulaya, tungependa kuiona Slovakia ikitoa kipaumbele kwa suala la kutumwa misaada ya dharura na kibinadamu kwa nchi mbili hizo za Kiarabu zinazokabiliwa na migogoro, katika vikao vya EU."
Wakati huo huo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema Tehran iko tayari kuboresha uhusiano wake na Bratislava katika kipindi hiki cha kutekelezwa makubaliano ya nyuklia yanayofahamika kama JCPOA.
kwa upande wake Rais wa Slovakia Andrej Kiska amesema kuwa, makubaliano hayo ya nyuklia kati ya Iran na nchi za kundi la 5+1 yanadhihirisha kuwa, jitihada za kidiplomasia zinaweza kuleta natija na mafanikio mbali mbali, kinyume na chaguo la vita na uhasama. Kadhalika amepongeza nafasi ya Iran katika eneo la Mashariki ya Kati na kuongeza kuwa, nchi yake iko tayari kuboresha uhusiano wa kiuchumi na Jamhuri ya Kiislamu.
Zarif aliwasili mjini Bratislava akiwa na ujumbe wa wafanyabiashara na wawekezaji jana usiku, katika ziara ya nchi tatu za Mashariki mwa Ulaya, ikiwemo Slovakia.