Hatua mpya ya Trump dhidi ya Waislamu
(last modified Sun, 29 Jan 2017 03:51:19 GMT )
Jan 29, 2017 03:51 UTC
  • Hatua  mpya ya Trump dhidi ya Waislamu

Kwa mujibu wa amri iliyotiwa saini na Rais Donald Trump wa Marekani chini ya anwani ya kulinda taifa mbele ya kuingia magaidi wa kigeni katika ardhi ya Marekani, ni marufuku kutolewa viza za kuingia Marekani kwa raia wa nchi ambazo eti zina madhara kwa maslahi ya Marekani kwa kipindi cha siku 90.

Amri hiyo inahusu raia wa nchi zisizopungua saba ambazo ni Iran, Iraq, Syria, Yemen, Libya, Sudan na Somalia. Amri hiyo pia imesimamisha mipango yote ya kuwapokea wahajiri na wahamiaji nchini Marekani kwa kipindi cha siku 120 na kupunguza kiwango cha kupokea wahamiaji kwa asilimia 50.

Kwa hakika Donald Trump amesaini amri hiyo katika fremu ya kutekeleza ahadi aliyotoa wakati wa kampeni za uchaguzi wa rais ya kuwazuia kabisa Waislamu kuingia Marekani. Kisingizio kilichotumiwa na Trump kusaini amri hiyo ni eti kuzuia watu wanaodhaniwa kuwa ni magaidi kuingia nchini Marekani. Hata hivyo linajitokeza swali kwamba, je, raia wa nchi hizo saba wameshiriki katika mashambulizi ya kigaidi yaliyotokea katika miaka kadhaa ya hivi karibuni nchini Marekani au la? Jibu la swali hilo ni kwamba, rekodi ya mashambulizi yaliyofanyika katika miaka kadhaa ya hivi karibuni nchini Marekani inaonesha kuwa, idadi kubwa ya magaidi waliofanya mashambulizi nchini Marekani ni raia wa nchi waitifaki na marafiki wa Marekani. Mfano wa wazi wa ukweli huo ni mashambulizi ya Septemba 11, mwaka 2001 katika miji ya Washinton na New York. Rekodi zinaonesha kuwa, magaidi 15 kati ya 19 waliotekeleza mashambulizi hayo walikuwa raia wa rafiki mkubwa wa Marekani yaani Saudi Arabia. Vilevile watu waliofanya mashambulizi ya Disemba 2 mwaka 2015 katika mji wa San Bernardino katika jimbo la California walikuwa mke na mume wa Kipakistani, na aliyefanya shambulizi la tarehe 12 Juni mwaka jana wa 2016 na kuua raia 50 alikuwa raia wa Afghanistan, ambazo zote hazikuwekwa kwenye orodha ya raia wanaozuiwa kuingia Marekani.

Trump amezidisha chuki na misimamo ya kibaguzi dhidi ya Uislamu na Waislamu

Kwa utaratibu huo inaonekana wazi kuwa, lengo halisi la amri iliyotiwa saini na Donald Trump si kuwazuia magaidi kuingia katika ardhi ya Marekani, bali ni kuzishinikiza zaidi nchi zenye uhusiano usio mzuri na serikali ya Washington na sera zake za chuki dhidi ya Uislamu na Waislamu.

Inaonekana kuwa, Donald Trump ametumia mashambulizi ya kigaidi yaliyotokea barani Ulaya katika miezi ya hivi karibuni kama kisingizio cha kutekeleza mipango yake ya kibaguzi dhidi ya Waislamu. Katika kampeni zake za uchaguzi wa rais, Trump alitangaza kuwa, iwapo angeshinda kiti hicho angewazuia kabisa Waislamu kuingia Marekani. Matamshi hayo ya kibaguzi yalikosolewa sana ndani na nje ya Marekani.

Ukweli ni kuwa, amri ya Rais Donald Trump ya kuzuia viza ya kuingia Marekani raia wa nchi kadhaa za Kiislamu imezidisha wasiwasi wa kuongezeka wimbi na hujuma dhidi ya Waislamu na Uislamu nchini Marekani. Nukta muhimu inayopaswa kuashiriwa hapa kuhusiana na madai ya Trump ni kwamba, ni idadi ngogo sana na Waislamu hususan huko Marekani wenye misimamo mikali, na wafuasi karibu wote wa dini hiyo ya Mwenyezi Mungu wanapinga misimamo ya kundi hilo dogo. Sasa je, ni insafu na uadilifu kuutuhumu Umma mzima wa Waislamu karibu bilioni mbili kwamba ni magaidi na wahalifu kwa sababu tu ya vitendo viovu vunavyofanywa na watu wachache miongoni mwao ambao si lolote wala chochote wakipimanishwa na idadi ya Waislamu kote duniani?

Waislamu wa Marekani

Kwa msingi huo inaonekana kuwa, hatua ya Donald Trump ya kusaini amri ya kuwazuia Waislamu kuingia Marekani ni kutoa adhabu kwa mamilioni ya wafuasi wa dini hiyo kutokana na vitendo vilivyofanywa na watu kadhaa tu miongoni mwao, suala ambalo lenyewe linatambuliwa kuwa ni dhulma, ugaidi na ubaguzi.            

Tags