Ufaransa na Ujerumani zahofia uwezekano wa kuvunjika Umoja wa Ulaya
https://parstoday.ir/sw/news/world-i25112-ufaransa_na_ujerumani_zahofia_uwezekano_wa_kuvunjika_umoja_wa_ulaya
Waziri Mkuu wa Ufaransa Bernard Cazeneuve ametaka kuwepo na mshikamano mkubwa zaidi kati ya nchi yake na Ujerumani kwa ajili ya kukabiliana na hatari ya kuvunjika Umoja wa Ulaya (EU).
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 14, 2017 04:03 UTC
  • Ufaransa na Ujerumani zahofia uwezekano wa kuvunjika Umoja wa Ulaya

Waziri Mkuu wa Ufaransa Bernard Cazeneuve ametaka kuwepo na mshikamano mkubwa zaidi kati ya nchi yake na Ujerumani kwa ajili ya kukabiliana na hatari ya kuvunjika Umoja wa Ulaya (EU).

Cazeneuve ametoa wito huo mjini Berlin, Ujerumani katika mkutano na waandishi wa habari aliofanya pamoja na Kansela Angela Merkel wa nchi hiyo.

Amesema ushirikiano kati ya Ujerumani na Ufaransa ni jambo la dharura ili kuweza kukabiliana na wimbi la sera za ufuataji maoni ya umma na hatari ya kusambaratika Umoja wa Ulaya.

Waziri Mkuu wa Ufaransa amesisitiza kuwa: "Mshikamano baina ya Paris na Berlin ni jambo lenye ulazima zaidi hivi sasa kuliko wakati mwengine wowote kwa sababu baadhi wamefanikiwa kuzusha hali ya mfarakano ndani ya Umoja wa Ulaya, na sisi tunakabiliwa na changamoto kubwa kadhaa za kimataifa."

Amezitaja baadhi ya changamoto na matatizo makubwa yanayoikabili Ulaya kuwa ni pamoja na mgogoro wa wakimbizi, hali tete ya usalama inayotokana na baa la ugaidi na masuala yanayohusiana na hifadhi ya mazingira.

Kwa upande wake, Kansela Angela Merkel wa Ujerumani amesema kuimarishwa uhusiano wa Ufaransa na Ujerumani hususan mitazamo ya pamoja ya kiuchumi kutandaa mazingira ya kujenga Ulaya imara na yenye nguvu.../