Nchi za Kiislamu zatakiwa kukabiliana na ugaidi wa kimitandao
Washiriki wa kongamano la kimataifa lililopewa jina la 'Nafasi ya Vyombo vya Habari katika Kupambana na Ugaidi' lililofanyika nchini Misri, wamesisitiza juu ya udharura wa kuwepo ushirikiano wa asasi za nchi za Kiislamu kwa lengo la kukabiliana na ugaidi wa kimtandao.
Kongamano hilo lililofanyika mjini Asyut, Misri kuanzia tarehe tatu hadi tano ya mwezi huu wa Machi, liliitishwa kwa lengo la kuvishawishi vyuo vikuu vya Kiislamu katika kukabiliana na wimbi la ugaidi chini ya ushirikiano wa kituo cha Utafiti wa Mustakbali nchini Misri. Mwishoni mwa kongamano hilo, washiriki wametoa ripoti ya pamoja juu ya umuhimu wa kubuni mkakati kwa ajili ya vyombo vya habari vya Kiislamu kwa ajili ya kupambana na hatari ya ugaidi ambao unatishia usalama wa mwanadamu kote duniani. Katika ripoti hiyo pia, kumesisitizwa juu ya ushirikiano wa asasi tofauti za nchi za Kiislamu kwa ajili ya kuchukua hatua za lazima na zenye taathira katika kukabiliana na wimbi hilo la ugaidi wa kimtandao, ambao ni moja ya nyenzo muhimu zinazotumiwa hivi sasa na makundi ya kigaidi kwa ajili ya kueneza mafundisho yao potofu kwa vijana. Aidha washiriki wamesisitizia udharura wa kuungwa mkono vyombo vya habari vya Kiislamu kwa ajili ya jamii ya watu wachache Waislamu ndani ya mataifa yasiyokuwa ya Kiislamu ili nao waweze kufaidika na mafundisho ya dini tukufu ya Kiislamu.