UN yaitaka Myanmar ikomeshe jinai zake dhidi ya Waislamu wa Rohingya
Umoja wa Mataifa umesema ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu dhidi ya Waislamu wa jamii ya Rohingya wa Myanmar umefikia kiwango cha kutia wasi wasi na ni mkubwa zaidi ya ilivyodhaniwa.
Yanghee Lee, Mjumbe wa UN aliyetumwa kuwatembelea Waislamu wa Rohingya waliokimbilia Bangladesh amesema simulizi alizopewa na wakimbizi hao wa Myanmar ni za kuhuzunisha na zinazoashiria ukubwa wa jinai za kutisha wanazofanyiwa wenzao waliobaki Myanmar.
Afisa huyo wa Umoja wa Mataifa amesema kuwa, wanawake Waislamu wa Rohingya wamemueleza jinsi wenzao walivyobakwa kwa umati na maafisa usalama wa Myanmar, baadhi yao wakichinjwa huku watoto wakitupwa kwenye moto mkali wakiwa hai.
Mapema mwezi huu, ripoti ya Umoja wa Mataifa ilivitaka vikosi vya usalama vya Myanmar vikomeshe jinai zake dhidi ya Waislamu wa Rohingya yakiwemo mauaji ya halaiki dhidi ya Waislamu hao.
Ripoti hiyo ya UN ilisema kuwa, mbali na mauaji na vitendo vya utumiaji mabavu vya vikosi vya usalama vya Myanmar dhidi ya Waislamu wa jamii ya Rohingya, vikosi hivyo vimefanya vitendo vya ubakaji, mateso na hata kuwatishia kwa silaha Waislamu wa jamii hiyo sambamba na kuwaua watoto wao.
Mabudha wenye misimamo ya kurufutu ada wamekuwa wakishirikiana na maafisa usalama wa Myanmar katika mauaji na ukandamizaji dhidi ya Waislamu wa kabila la Rohingya katika mkoa wa Rakhine kwa muda sasa, huku hujuma hizo zikishadidi tokea mwaka 2012.