Uturuki yaituhumu Ujerumani kuwa inaunga mkono ugaidi
https://parstoday.ir/sw/news/world-i25914-uturuki_yaituhumu_ujerumani_kuwa_inaunga_mkono_ugaidi
Katika kile kinachoonekana ni kuzidi kuingia doa uhusiano wa Ankara na Berlin, Rais wa Uturuki ameituhumu Ujerumani kuwa inaunga mkono ugaidi.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 04, 2017 03:40 UTC
  • Uturuki yaituhumu Ujerumani kuwa inaunga mkono ugaidi

Katika kile kinachoonekana ni kuzidi kuingia doa uhusiano wa Ankara na Berlin, Rais wa Uturuki ameituhumu Ujerumani kuwa inaunga mkono ugaidi.

Akiongea mjini Istanbul jana Ijumaa, Recep Tayyip Erdogan, Rais wa Uturuki amesema Ujerumani inafaa kuwekwa kwenye mizani kwa kuyapa himaya na kuyaunga mkono makundi ya kigaidi.

Matamshi ya Erdogan yanaonekana kuwa radiamali kwa hatua ya Ujerumani kufuta mikutano ya hadhara na kampeni za kuunga mkono kura ya maoni ya Uturuki kufanyika nchini humo. Wadadisi wa mambo wanasema kura hiyo ya maoni inapania kumpa mamlaka zaidi Rais Erdogan.

Kansela wa Ujerumani alipoitembelea Uturuki mwezi jana

Hivi karibu baadhi ya wabunge wa Ujerumani walimtaka Kansela wa nchi hiyo Angela Merkel kutomruhusu Erdogan kuingia nchini humo kuipigia debe kura hiyo ya maoni.

Kabla ya hapo, Wizara ya Mambo ya Nje ya Uturuki ilimuita Balozi wa Ujerumani mjini Ankara, kulalamikia hatua ya serikali ya Berlin kufuta kampeni za kuunga mkono kura ya maoni ya Uturuki nchini humo.

Mkwaruzano kati ya Ankara na Berlin ulianza baada ya jaribio la mapinduzi lililofeli Julai mwaka jana, ambapo serikali ya Uturuki inazituhumu baadhi ya nchi za Magharibi kuhusika nalo.