Korea Kusini yakanusha kusitisha uwekaji ngao ya makombora THAD
Msemaji wa Wizara ya Ulinzi nchini Korea Kusini amesema kuwa, ripoti za baadhi ya vyombo vya habari juu ya kusitishwa mpango wa uwekaji ngao ya Marekani ya makombora katika ardhi ya nchi hiyo hadi baada ya uchaguzi, hayana ukweli wowote.
Moon Sung-Keun amesema kuwa, habari ambazo zimekuwa zikitolewa kwamba zoezi la kuweka ngao hiyo ya makombora ya THAD limesimamishwa kutokana na sababu za kisiasa, hazina ukweli wowote. Ameongeza kuwa, hadi sasa hakuna mabadiliko yoyote katika kadhia ya uwekaji wa ngao hiyo ya makombora baina ya Korea Kusini na Marekani na kwamba, suala hilo linaendelea kwa kasi kama ilivyopangwa.
Washington na Seoul zilikubaliana kuweka ngao hiyo ya makombora ya THAD mwezi Julai mwaka jana, huku zoezi hilo likianza mwanzoni mwa mwezi huu wa Machi. Hii ni katika hali ambayo baadhi ya vyombo vya habari vilikuwa vimetangaza kwamba, suala la uwekaji ngao hiyo litajadiliwa katika mazungumzo ya Rais Donald Trump wa Marekani na Rais Xi Jinping wa China mwanzoni mwa mwezi April ujao na kwamba kuna uwezekano kadhia hiyo itaendelea kusitishwa hadi tarehe tisa Mei mwaka huu, baada ya uchaguzi wa rais nchini Korea Kusini.