Ukungu wa giza wa uchaguzi wa rais nchini Ufaransa
Shambulizi la kigaidi lililofanyika majuzi katika mtaa wa Champs-Élysées mjini Paris, Ufaransa siku kadhaa kabla ya uchauzi wa rais wa nchi hiyo si tu kwamba umezidisha anga ya kipolisi nchini humo, bali pia limezidisha wingu la giza kuhusu matokeo ya uchaguzi huo kwa kuathiri kiwango cha uungaji mkono wa raia kwa wagombea wa nafasi hiyo.
Uchunguzi wa maoni unaoesha kuwa, kiwango cha uungaji mkono wa wananchi wa Ufaransa kwa mgombea urais wa mrengo wenye misimamo mikali ya kulia Marine Le Pen kimeongezeka kwa asilimia 1 baada ya shambulizi hilo na kufikia asilimia 23. Sambamba na hayo kiwango cha uungaji mkono wa Wafaransa kwa Emmanuel Macron, mgombea wa kujitegemea ambaye anatajwa kuwa na nafasi nzuri zaidi ya kushinda uchaguzi huo, kimeshuka kwa nusu asilimia na kufikia asilimia 24.5.
Wakati huo huo Rais Donald Trump wa Marekani amesema kuwa shambulizi la Champs-Élysées limemfaidisha Marine Le Pen. Inaonekana kuwa shambulizi hilo limekuwa tuzo ya ghafla kwa mgombea huyo wa mrengo wenye misimamo mikali wa kulia ambaye ametumia tukio hilo kama fursa ya kueneza zaidi propaganda zake za uchaguzi kama nara yake ya kuzidishwa mapambano dhidi ya wahajiri hususan Waislamu kwa kisingizio cha kupambana na ugaidi nchini Ufaransa. Marine Le Pen ameashiri shambulizi hilo la Paris na kuituhumu serikali ya kisoshalisti ya Ufaransa kuwa imeshindwa kupambana na ugaidi. Madai hayo yamekabiliwa na majibu makali ya serikali ya sasa ya nchi hiyo.

Waziri Mkuu wa Ufaransa, Bernard Cazeneuve ametetea utendaji wa vyombo vya usalama vya serikali ya nchi hiyo na kumtuhumu Marine Le Pen kuwa ametumia kisiasa shambulizi la kigaidi la Paris. Cazeneuve amesema, Marine Le Pen amekosa haya kwa kutumia vibaya hofu na hisia za Wafaransa.
Alaa kulli hal, hatuwezi kukana kwamba, shambulizi la kigaidi la Champs-Élysées si tu kwamba limezidisha mtazamo mbaya wa Wafaransa kwa serikali ya nchi hiyo, bali pia limetayarisha mazingira ya watu kuelekea upande wa Marine Le Pen. Hii ni pamoja na kuwa, woga wa kukaririwa shambulizi kama hilo hii leo wakati wa zoezi la uchaguzi yumkini ukawa na taathira katika kiwango cha ushiriki wa wananchi katika uchaguzi huo.
Pamoja na hayo yote iwapo Marine Le Pen atashinda uchaguzi wa Rais wa Ufaransa ambao inatabiriwa kuwa utaingia duru ya pili, huo utakuwa mwanzo wa awamu mpya katika historia ya sasa ya Ufaransa. Hasa iwapo ngombea huyo mwenye misimamo mikali atatekeleza wito wake wa kujiondoa Ufaransa katika Umoja wa Ulaya (Frencexit), suala ambalo litakuwa sawa na mwisho wa umoja huo na matunda yake ya miongo kadhaa.
Pamoja na hayo yote, Marine Le Pen anakabiliana na mpinzani mkubwa yaani Emmanuel Macron, ambaye bado anaongoza katika uchunguzi wa maoni. Kwa utaratibu huo na licha ya kwamba uungaji mkono wa Le Pen umeongezeka baada ya shambulizi la Paris, lakini wachambuzi wa mambo bado wanaamini kuwa, Emmanuel Macron ataibuka na ushindi katika duru zote mbili za uchaguzi wa rais nchini Ufaransa.
Nafasi za wagombea wengine katika uchaguzi wa leo wa Ufaransa bado hazijajulikana vyema na zimekuwa zikipanda na kushuka kila kukicha. Uchunguzi wa maoni uliofanyika hivi karibuni umeonesha kuwa, kila mmoja kati ya Francois Fillon wa mrengo wa kulia kati na Jean-Luc Melenchon wa mrengo wenye siasa kali za kushoto wamepata asimia 19 za kura.
Kwa ujumla, kwa kutilia maanani kampeni zinazofanyika na pia matokeo yake, tunaweza kusema kuwa, uchaguzi wa leo wa rais nchini Ufaransa ni miongoni mwa matukio ya kisiasa yenye umuhimu mkubwa barani Ulaya katika mwaka huu wa 2017.