HRW: India iwazuie Wahindu wanowaua Waislamu wenye kuchinja ng'ombe
Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch (HRW) limeitaka serikali ya India ichukue hatua kuzuia mauaji yanayofanywa na Wahindu dhidi ya Waislamu kwa sababu tu wanachinja ng'ombe.
Katika taarifa yake ya jana Ijumaa, HRW imelaani vikali magenge ya wafuasi wa dini ya Kihindu wanaodai kuwa eti ni walinzi wa ng'ombe ambao wanawahujumu na kuwaua Waislamu na watu wa daraja la chini katika jamii kwa sababu tu wanauza, kununua au kichinja ng'ombe kwa ajili ya nyama.
HRW imesema tokea Waziri Mkuu Narendra Modi aingie madarakani mwaka 2015 hadi sasa, karibu Waislamu 10 wameshauliwa na magenge ya Wahindu wanaowashambulia kwa sababu tu ya kuchinja ng'ombe kwa ajili ya nyama.
Ingawa Modi amelaani hujuma hizo, lakini serikali yake inalaumiwa kwa kutochukua hatua za kutosha za kuzuia mauaji ya Waislamu. Magenge ya Wahindu wenye misimamo mikali kutoka chama tawala cha Bharatiya Janata wanawashambulia Waislamu kwa sababu tu wanachinja ngombe ambapo kwa mujibu wa itikadi za dini ya Kihindu na Kibaniani, ng'ombe ni mnyama mtakatifu na wanapinga kuchinjwa kwa ajili ya nyama.