Zarif akutana na Waziri Mkuu wa Thailand mjini Bangkok
Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran, Muhammad Javad Zarif amekutana na kufanya mazungumzo na Prayut Chan-o-cha, Waziri Mkuu wa Thailand jijini Bangkok, kuhusu uhusiano wa pande mbili.
Katika siku ya pili ya safari yake nchini Thailand, Zarif amepokewa na Waziri Mkuu wa nchi hiyo katika Jumba la Serikali na wawili hao wamejadiliana kuhusu masuala ya nchi mbili hizi na umuhimu wa kuimarisha uhusiano wa Bangok na Tehran katika nyuga tofauti, hususan za kisiasa na kiuchumi.
Jana jioni, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran alifanya mazungumzo na mwenzake wa nchi hiyo Don Pramudwinai kuhusu uhusiano wa pande mbili na wa kieneo. Zarif ameitembelea nchi hiyo kwa minajili ya kushiriki katika Mkutano wa 14 wa Mawaziri wa Bara Asia kuhusu masuala ya ushirikiano. Akihutubia mkutano huo hapo jana, Muhammad Javad Zarif alisisitizia umuhimu wa ushirikiano miongoni mwa nchi za eneo hilo kwa shabaha ya kushinda vita dhidi ya ugaidi na misimamo ya kufurutu ada.
Kabla ya ziara ya Bangkok, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran alizitembelea Indonesia, Singapore na Brunei. Anazamiwa kuelekea New Zealand na Australia katika duru ya mwisho ya safari yake.