Malalamiko ya raia wa Korea Kusini dhidi ya Marekani
https://parstoday.ir/sw/news/world-i29862-malalamiko_ya_raia_wa_korea_kusini_dhidi_ya_marekani
Raia wa Korea Kusini wamefanya maandamano makubwa katika miji tofauti ya nchi hiyo hususan Seoul, mji mkuu wa taifa hilo ambapo mbali na kutaka kusimamishwa haraka uwekaji ngao ya makombora ya Marekani THAAD, wametaka pia kusitishwa hatua za kijeshi za askari wa nchi hiyo katika eneo la Korea.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Jun 01, 2017 03:19 UTC
  • Malalamiko ya raia wa Korea Kusini dhidi ya Marekani

Raia wa Korea Kusini wamefanya maandamano makubwa katika miji tofauti ya nchi hiyo hususan Seoul, mji mkuu wa taifa hilo ambapo mbali na kutaka kusimamishwa haraka uwekaji ngao ya makombora ya Marekani THAAD, wametaka pia kusitishwa hatua za kijeshi za askari wa nchi hiyo katika eneo la Korea.

Kwa kuzingatia kuwa serikali mpya ya Korea Kusini pia haikubaliani na uwekaji ngao hiyo ya makombora nchini humo, ndio maana malalamiko ya wananchi kuhusiana na suala hilo yanazidi kuongezeka. Kabla ya hapo pia Wakorea Kusini walikusanyika katika maeneo ya jirani na mji wa Seongju ulioko kilometa 300 kutoka mji wa Seoul, wakitaka kuondolewa vifaa vya ngao hiyo iliyoanza kusimikwa na Wamarekani nchini humo. Malalamiko ya raia wa taifa hilo juu ya suala la ngao hiyo tajwa yamefanyika kwa sababu kadhaa. Mosi ni kwamba, kwa mtazamo wa hifadhi ya mazingira, inaelezwa kuwa ngao ya makombora ya THAAD ni yenye madhara makubwa kwa mazingira yanayoizunguka. Pili ni kwamba, kwa mujibu wa wataalamu wa Uchina na Russia, ngao hiyo ya kisasa ya Marekani, sio mfumo kamili ambao unaweza kuidhaminia usalama nchi yote ya Korea Kusini na badala yake itaigharimu Seoul kiasi kikubwa cha gharama katika kudhamini fedha za uendeshaji wake.

Wakorea Kusini wakionyesha hasira zao juu ya Marekani

Ni kwa ajili hiyo ndio maana Kim Jin-Hyung, mmoja wa mawakili wa Korea Kusini kutoka taasisi ya 'Mawakili kwa ajili ya Jamii ya Kidemokrasia' nchini humo akanukuliwa akisema kama ninavyonukuu: "Kwa upande wa kisheria ngao ya THAAD itakumbwa na changamoto nyingi hasa kwa kuwa inatishia usalama wa kitaifa wa Korea Kusini. Kwa ajili hiyo taasisi ya mawakili nchini imeamua kuanzisha changamoto moja ya kikatiba na kufungua mashitaka ya kisheria kuhusiana na suala hilo. Hii ni kwa kuwa katiba ya Korea Kusini inasisitiza kuwa raia wote wa nchi hii wanayo haki ya kuwa na usalama wa mazingira na hii ni katika hali ambayo uwekaji ngao hiyo ya makombora unakinzana na katiba na haki ya usalama wa wananchi katika suala la mazingira." Mwisho wa kunukuu.

Wakorea Kusini na upinzani wao kwa Marekani

Ama changamoto ya tatu inayowafanya raia wa Korea Kusini kupinga uwekaji ngao ya kisasa ya makombora ya Marekani aina ya THAAD nchini mwao, ni upinzani mkubwa wa kieneo na kimataifa ambao pia utasababisha kutia doa mahusiano ya nchi yao na majirani zake ikiwemo Uchina. Kiasi kwamba serikali ya Beijing na katika kulalamikia suala hilo imeamua kuiwekea vikwazo vya kiuchumi na utalii Korea Kusini, suala ambalo limekuwa na matokeo mabaya kwa sekta ya uchumi na viwanda ya Korea Kusini. Mbali na suala la kujikinga na mashambulizi tarajiwa ya Korea Kaskazini, lakini Wakorea Kusini wanaamini kuwa, malengo ya Marekani ya kuweka ngao hiyo nchini mwao ni zaidi ya yale yanayotolewa na Washington.

Moja ya meli za kivita za Marekani zilizotumwa eneo la Korea

China kwa kufahamu ukweli huo, ndio maana ikafuata misimamo mikali katika kupinga ujenzi wa ngao tajwa na katika hilo haipo tayari kabisa kulegeza msimamo wake. Kuhusiana na hilo na katika kuvunja hoja na kisingizio cha Marekani cha kuweka ngao hiyo kupitia nara ya kuitaja Korea Kaskazini kuwa tishio na pia njama za Washington za kujiimarisha kijeshi eneo la Peninsula ya Korea, ndipo Beijing ikaitaka Pyongyang kuandaa mazingira kwa ajili ya kuanza mazungumzo na jirani yake Seoul yenye lengo la kuhitimisha mgogoro wa eneo hilo. Ndio maana wataalamu wa China wakanukuliwa wakisema: "Viongozi wa Beijing wanajitahidi kuwashawishi viongozi wa Pyongyang kuachana na siasa za makabiliano na badala yake kupata misaada ya kiuchumi. Hii ikiwa na maana kwamba, China haifurahishwi na majaribio ya kila mara ya makombora ya Pyongyang na kadhalika siasa za kijeshi za Marekani katika eneo." Mwisho wa kunukuu.

Wakati Marekani ilipokuwa ikiingiza vifaa vya ngao ya THAAD ilikutana na maandamano haya

Kwa kuzingatia kuwa uchumi wa nchi za eneo la mashariki mwa Asia unategemea uzalishaji, hivyo mataifa hayo hayapendelei kuona hali ya mambo ikizorota katika eneo na ni kwa msingi huo ndio maana zinafanya juhudi ya kutatua mgogoro huo, sambamba na kuhitimisha siasa za Marekani za kuifanya Uchina na Korea Kaskazini kuwa tishio ili kurejesha utulivu katika eneo hilo. Inaonekana kuwa Korea Kusini pia inataraji kuiona Beijing ikiishawishi Pyongyang ili kusimamisha miradi yake ya makombora na silaha za nyuklia ili kwa njia hiyo Seoul iweze kuhitimisha uwepo wa kijeshi wa Marekani katika Peninsula ya Korea. Kwa kuzingatia kuwa nara ya Rais Moon Jae-in wa Korea Kusini ya kutatua tofauti na Uchina na kadhalika kuamiliana na Korea Kaskazini ndizo zilizomfanya ashinde uchaguzi wa hivi karibuni nchini humo, hivyo ushirikiano wa Beijing na Seoul mbali na kusaidia utekelezaji wa nara hizo, utawezesha pia kuipa nguvu dhana ya mazungumzo na maelewano katika eneo badala ya mivutano na utumizi wa nguvu za kijeshi, suala ambalo litafuta kisingizio kinachotumiwa na Marekani na kuifanya ilazimike kuondoa askari na zana zake za kijeshi katika Peninsula ya Korea.