Kuongezeka hasira za Wabahrain dhidi ya Marekani
https://parstoday.ir/sw/news/world-i29954-kuongezeka_hasira_za_wabahrain_dhidi_ya_marekani
Habari kutoka nchini Bahrain zinaonesha kuongezeka mno hasira za wananchi wa nchi hiyo dhidi ya Marekani kutokana na siasa zake za kuunga mkono ukandamizaji unaofanywa na utawala wa Aal Khalifa dhidi ya raia hususan kuendelea kuzingirwa nyumba ya Sheikh Isa Qassim kwa baraka kamili za Marekani.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 02, 2017 21:58 UTC

Habari kutoka nchini Bahrain zinaonesha kuongezeka mno hasira za wananchi wa nchi hiyo dhidi ya Marekani kutokana na siasa zake za kuunga mkono ukandamizaji unaofanywa na utawala wa Aal Khalifa dhidi ya raia hususan kuendelea kuzingirwa nyumba ya Sheikh Isa Qassim kwa baraka kamili za Marekani.

Viongozi wa harakati ya Februari 14 ya Bahrain wamesema kuwa, wananchi wa nchi hiyo wanaitaka Marekani iondoe wanajeshi wake nchini humo kutokana na siasa zake za kuunga mkono uvamizi uliofanywa na askari wa ukoo wa kifalme katika nyumba ya Sheikh Isa Qassim, mwanachuoni mkubwa wa Kishia wa nchi hiyo. 

Esam al Manami, mmoja wa viongozi wa harakati ya Februari 14 ya Bahrain amesisitiza kuwa, umoja wa vijana wa harakati hiyo wameamua kuitangaza Ijumaa ya mwanzo ya mwezi mtukufu wa Ramadhani kuwa siku ya taifa ya kuwafukuza wanajeshi wa Marekani nchini Bahran na kulilazimisha dola hilo la kibeberu kuondoa kambi yake nchini humo. Kitendo cha Marekani cha kutuma wanajeshi wake nchini Bahrain ni uvunjaji wa wazi wa haki ya kujitawala Bahrain na ndio maana jambo hilo linalalamikiwa sana na wananchi wa nchi hiyo ya Kiarabu.

Maandamano ya kumuunga mkono Sheikh Isa Qassim nchini Bahrain

 

Utawala wa Bahrain umeongeza ukandamizaji wake dhidi ya raia wa nchi hiyo baada ya kushiriki katika kikao cha Riyadh, Saudi Arabia na kupata baraka za Rais wa Marekani, Donal Trump.

Wachambuzi wa mambo wanasema kuwa, kitendo cha askari wa utawala wa Aal Khalifa cha kuivamia nyumba ya Sheikh Isa Qassim ulikuwa ni ujumbe wa kwanza wa kuonesha kuwa baadhi ya nchi za Kiarabu na Marekani zinashirikiana kufanya ukandamizaji dhidi ya wananchi wa Bahrain. Tangu mwezi Februari 2011, Bahrain ilikuwa uwanja wa mapinduzi ya wananchi dhidi ya utawala wa kiimla wa ukoo wa Aal Khalifa. Wananchi wa Bahrain walikaribia mno kufanikisha mapinduzi yao dhidi ya utawala huo wa kidikteta, hata hivyo nchi za Saudia na Imarati zilituma wanajeshi wao huko Bahrain kwenda kukandamiza mapinduzi hayo ya wananchi. Hata hivyo hadi leo hii wameshindwa kuvunja harakati hizo za wananchi Waislamu wa Bahrain. Ukandamizaji wote huo unafanyika kwa baraka kamili za madola ya kibeberu hususan Marekani ambayo yanafanya kila liwezekanalo kuhakikisha tawala za kiimla za vibaraka wao zinaendelea kubakia madarakani katika nchi hizo za Kiarabu. 

Moja ya mambo yanayowakasirisha mno wananchi wa Bahrain ni kuona madola ya kibeberu kama vile Marekani yanadhibiti mambo yote ya kisiasa, kijeshi na kiuchumi ya nchi yao. Kambi za kijeshi za madola ya kibeberu zimeoingezeka kwenye nchi hiyo ndogo ya Kiarabu na kila leo ukandamizaji dhidi ya raia wasio na hatia unakuwa mkubwa zaidi. 

Ukatili dhidi ya raia wa Bahrain umeongezeka baada ya Donald Trump kutembelea Saudi Arabia na kuonana na ukoo wa kifalme wa Bahrain

 

Mwaka 1971, Bahrain ilitiliana saini na Marekani makubaliano maalumu ya kijeshi. Baada ya kutiwa saini makubaliano hayo, nchi ndogo ya Bahrain ilimega eneo lenye ukubwa wa kilomita mraba 40 za ardhi yake na kuipa Marekani. Mwaka 1993 kambi kubwa ya jeshi la majini la Marekani ilianzishwa nchini Bahrain na mwaka 1995 nchi hiyo ya Kiarabu ikawa rasmi kituo kikubwa cha kijeshi cha Marekani kupitia kuanza rasmi kazi za Kikosi cha Tano cha Jeshi la Majini la nchi hiyo ya kibeberu.

Tangu mwanzoni mwa harakati yao mwaka 2011, wananchi wa Bahrain wamekuwa wakitaka kufutwa makublianao hayo ya kuidhalilisha Bahrain mbele ya Marekani. Kwa kweli mkataba huo wa kijeshi wa Marekani na Bahrain unaonesha wazi tangu ulipotiwa saini kwamba, lengo lake ni kukitumia kisiwa cha Bahrain kama dungu la kijeshi kwa ajili ya kuingiia masuala ya ndani ya nchi za eneo hili.

Zaidi ya hayo ni kwamba harakati ya wananchi wa Bahrain imeshuhudia umwagaji mkubwa wa damu unaofanywa na askari wa ukoo wa Aal Khalifa kwa kushirikiana na mamluki wa Saudi Arabia na kwa baraka kamili za kijeshi na kisiasa za Marekani. Bila ya shaka ni kwa sababu hiyo ndio maana wananchi wa Bahrain wakaiona Marekani kuwa ndiye chanzo kikuu cha matatizo yao yote, hivyo kuongezeka hasira zao dhidi ya dola hilo la kibeberu, bila ya shaka yoyote ni radiamali ya kawaida kabisa ya kila anayedhulumiwa.