Jun 18, 2017 03:50 UTC
  • Trump na maonyesho ya kusimama kidete mbele ya Cuba

Rais Donald Trump wa Marekani amefuta sehemu ya mapatano yaliyofikiwa kati ya Washington na Havana wakati wa utawala wa Rais Barack Obama ikiwa ni katika juhudi za kutekeleza ahadi alizotoa wakati wa uchaguzi.

Akiwa Miami eneo wanapoishi Wacuba wengi wanaopinga mapinduzi ya nchini kwao, Rais huyo wa Marekani ameyataja makubaliano yaliyofikiwa kati ya Washington na Havana kuwa ya kutisha na kisha kufuta sehemu ya mapatano hayo. Huku akidai kuwa faida inayopatikana kufuatia kuboreka ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara kati ya Marekani na Cuba huishia katika mifuko ya wanajeshi wa Cuba, Trump sasa ameweka sheria ambazo zitabana shughuli za kibiashara na safari za raia wa nchi mbili hizo. Kwa mfano tokea sasa  raia wa Marekani walio na nia ya kusafiri nchini Cuba kwa malengo ya kitalii watakabiliwa na vizuizi kadhaa na pia kubanwa katika kusafirisha dola za Kimarekani kuelekea Cuba.

Rais Donald Trump wa Marekani akizungumza karibuni huko Miami 

Hata hivyo kinyume na matarajio ya makundi ya Wacuba wanaopinga mapinduzi na makundi yenye misimamo mikali ndani ya chama cha Republican, Trump hajarejesha uhusiano kati ya Marekani na Cuba katika hali iliyokuwepo kabla ya mwaka 2014. Mwaka 2014, Barack Obama Rais wa wakati huo wa Marekani alikutana na kufanya mazungumzo na Rais Raul Castro wa Cuba katika mazishi ya mzee Nelson Mandela mpinzani mkuu wa mfumo wa ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini. Mazungumzo hayo yalikuwa mwanzo wa kubadilika siasa za uhasama za nusu karne za Marekani mkabala na Cuba. Katika kuendeleza njia hiyo, viongozi wa nchi mbili hizo walitayarisha njia ya kuanzisha uhusiano kamili wa kidiplomasia na kufungua balozi zao katika nchi ya pili; ambapo hatimaye mazungumzo hayo yalipelekea kufanyika safari ya Barack Obama mjini Havana mwaka 2016. 

Barack Obama Rais mstaafu wa Marekani alipokutana na Rais Raul Castro wa Cuba nchini Afrika Kusini

Pamoja na hayo yote, vikwazo vya kiuchumi vya Marekani dhidi ya Cuba havijaondolewa kikamilifu licha ya mapatano ya pande mbili. Warepublican waliokuwa wakidhibiti Kongresi wakati wa utawala wa Rais Barack Obama walifanya juhudi kukwamisha kufutwa kikamilifu vikwazo vya miaka 50 vilivyowekwa na Marekani kwa Cuba. Kundi hilo lilikuwa likisisitiza kwamba hali ya mivutano iliyopo  kati ya Washington na Havana haipasi kupatiwa ufumbuzi madhali Wakomonisti wanaendelea kushika hatamu za uongozi huko Cuba; na wakat huo huo Havana kushindwa kutekeleza mabadiliko yanayotakiwa na Washington. Baada ya ushindi wa Trump katika uchaguzi wa Marekani, Wacuba wanaopinga mapinduzi na waitifaki wao wa Kihafidhina nchini Marekani walipata matumaini makubwa ya kurejeshwa uhusiano wa nchi hizo katika kipindi cha kabla ya kuondolewa mivutano. Wapinzani hao walitaraji kuwa, uhusiano wa nchi mbili hizo ungekatwa tena; na ushirikiano wowote wa kiuchumi na kibiashara kati ya Washington na Havana kuwekwa kando. 

Pamoja na hayo yote, kurejea Cuba katika siasa za vikwazo kamili vya kiuchumi vya Marekani halitakuwa jambo rahisi si kwa mtazamo wa kisiasa wala kiuchumi. Kwa upande wa kisiasa, kukata uhusiano na nchi kama Cuba ambayo ina ushawishi miongoni mwa nchi za kundi la kikanda kwa jina la ALBA za Amerika ya Latini kutapelekea kutengwa Washington. Hasa ikitiliwa maanani kuwa katika kukaribia kuingia katika muongo wa tatu katika karne ya 21 hakuna dhamana yoyote kwamba waitifaki wa Marekani watatekeleza siasa za uhasama za zamani dhidi ya Cuba. Isitoshe, hatua ya kusitisha ushirikiano wa kiuchumi na Cuba inahatarisha maelfu ya fursa za kazi nchini Marekani. Ni kwa sababu hii ndio maana Trump akafadhilisha kubakisha fremu kuu ya kuondolewa hali ya mvutano kati ya Washington na Havana ili kuishinikiza serikali ya Havana kwa upande mmoja na kuwaridhisha Wacuba wanaopinga mapinduzi wanaoishi Marekani pamoja na kundi la Warepublican wa nchi hiyo kwa upande wa pili.

Tags