Sisitizo la Macron la kubadilika siasa za Ufaransa mkabala na Syria
Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa alisisitiza Jumatano wiki hii kwamba kumuondoa madarakani Rais Bashar al Assad wa Syria si jambo linalopewa kipaumbele tena na Ufaransa kama njia ya kuupatia ufumbuzi mgogoro wa nchi hiyo. Macron amebainisha kuwa nchi yake hivi sasa inatoa kipaumbele kwa suala la kupambana na ugaidi huko Syria.
Rais Macron amefafanua kwamba kumuondoa madarakani Rais Bashar Assad hakuhesabiwi tena kuwa moja ya masharti kwa sababu hakuna mtu mwingine anayeweza halalishwa kuchukua nafasi yake. Kukiri huko kwa rais wa Ufaransa; nchi ya pili ndani ya Umoja wa Ulaya kuhusu kuwekwa kando lengo kuu la huko nyuma la Paris mkabala na kadhia ya Syria, yaani kumuondoa madarakani Bashar al Assad na kutamka bayana kuwa hakuna shakhsia halali anayeweza kuziba nafasi ya Assad, bila shaka kunathibitisha siasa na misimamo ya Russia na waitifaki wengine wa serikali halali ya Syria kuhusu hatua zisizo sahihi za nchi za Magharibi katika kushughulikia mgogoro wa Syria. Kwa kuzingatia vitisho vikubwa vya magaidi wa kitakfiri dhidi ya nchi za Ulaya khususan Ufaransa, Rais wa nchi hiyo amesisitiza kuwa hakuna kitu kilicho na taathira zaidi kuliko mapambano dhidi ya magaidi; na katika njia hiyo, akasema kuna ulazima wa kushirikiana pande zote khususan na Russia. Akiendelea na hotuba yake, Rais Macron ametangaza wazi kipaumbele chake kingine kuwa ni kuzuia kusambaratika Syria na kusisitiza juu ya ulazima wa kuwepo ramani ya njia ya kisiasa na kidiploasia kwa ajili ya kutatua mgogoro wa Syria.
Naye Kareem Pakzad mtafiti katika Taasisi ya Uhusiano wa Kimataifa na Kistratejia ya nchini Ufaransa amesema, Macron anaamini kuwa mapambano dhidi ya Daesh ni moja ya vipaumbele vya Ufaransa. Aidha kuhusiana na Syria, rais huyo wa Ufaransa anaamini kuwa suala la kumuengua madarakani Assad halipasi kutajwa kuwa ni sharti la kufanya mazungumzo ya amani, na wakati huo huo Bashar Assad hapaswi kuuungwa mkono.
Ufaransa na Uingereza ambazo ni nchi mbili muhimu na zenye taathira za Ulaya kuanzia mwaka 2011 zilianza kuelekeza jitihada zao katika malengo jumla ya muungano wa nchi za Magharibi na Kiarabu ili kuing'oa madarakani serikali halali ya Syria kwa kutoa misaada ya pande zote kwa makundi mbalimbali ya kigaidi yanayobeba silaha, ili kufikia lengo lao yaani kuipindua serikali ya Rais Bashar al Assad wa nchi hiyo. Ni wazi kuwa, Lengo kuu zaidi la nchi hizo lilikuwa ni kutoa pigo kwa mhimili mkuu wa muqawama katike eneo la Mshariki ya Kati yaani Syria; na hivyo kupelekea kusambaratika Syria, mnyororo wa muqawama katika eneo, na kisha kusababisha kutengwa na kuidhofisha Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Hizbullah ya Lebanon. Hasa ikizingatiwa kwamba kwa mtazamo wa nchi hizo, kama Syria ingesambaratika, nafasi ya Iran katika eneo la Mashariki ya Kati pia ingepata pigo na nchi hiyo kutengwa.
Pamoja na hayo yote, kuanzisha vita hivyo vya ndani hakukuwa na natija yoyote kwa Muungano huo wa nchi za Magharibi na zile za Kiarabu. Kwani hivi sasa mlingano wa nguvu huko Syria upo kikamilifu kwa maslahi ya serikali ya nchi hiyo na waitifaki wake. Katika hali ambayo nafasi ya makundi ya kitakfiri yenye silaha imedhoofika kikamilifu, khususan baada ya kukombolewa Halab yaani Aleppo; na jeshi la Syria na waitifaki wake kupata ushindi mwingine mwingi mashariki mwa nchi; serikali ya Syria pamoja na waitifaki wake yaani Russia, Iran na harakati ya Hizbullah hivi sasa zinakamilisha mchakato wa kuibuka na ushindi mwingine katika maeneo mbalimbali ya nchi hiyo. Wakati huo huo nchi za Ulaya ikiwemo Ufaransa zinatatizwa na kutiwa wasiwasi pakubwa na harakati za kigaidi na vitisho kutoka kundi la kitakfiri la Daesh; na katika uwanja huo Rais Macron wa Ufaransa anasisitiza suala muhimu yaani mapambano dhidi ya ugaidi huko Syria.
Hii ni katika hali ambayo serikali ya Syria na nchi waitifaki khususan Russia zimesisitiza mara kadhaa kwamba hakuna shakhsia anayefaa na halali anayeweza kuongoza serikali ya Syria badala ya Rais Assad na kwamba Syria itatumbukia katika vita vikubwa vya ndani kati ya makundi ya kitakfiri kwa ajili ya kushikilia madaraka iwapo makundi hayo yataibuka na ushindi. Kwa msingi huo, Rais Macron wa Ufaransa amezungumzia kubadilika siasa za Ufaransa mkabala na mgogoro wa Syria na kusisitiza kuendelea kusalia madarakani Bashar al Assad na kuendeshwa mapambano dhidi ya ugaidi nchini humo kinyume na msimamo wake wa huko nyumba kuhusu mgogoro wa Syria baada ya kushika hatamu za uongozi.