Uchunguzi: Uislamu unaenea kwa kasi nchini Australia
https://parstoday.ir/sw/news/world-i31064-uchunguzi_uislamu_unaenea_kwa_kasi_nchini_australia
Matokeo ya uchunguzi mpana na mkubwa wa maoni uliofanyika nchini Australia yanaonesha kasi kubwa ya watu kuelekea na kuingia kwenye dini tukufu ya Kiislamu nchini humo.
(last modified 2026-02-22T02:21:18+00:00 )
Jun 28, 2017 07:25 UTC
  • Uchunguzi: Uislamu unaenea kwa kasi nchini Australia

Matokeo ya uchunguzi mpana na mkubwa wa maoni uliofanyika nchini Australia yanaonesha kasi kubwa ya watu kuelekea na kuingia kwenye dini tukufu ya Kiislamu nchini humo.

Matokeo ya uchunguzi huo wa maoni uliofanywa mwaka jana na Idara ya Takwimu nchini Australia na kutangazwa jana Jumanne yanaonyesha kwamba, idadi ya watu wenye hamu ya kuingia kwenye dini nyingine zisizo Ukristo ikiwemo dini tukufu ya Kiislamu imeongezeka kwa kiasi kikubwa. Matokeo hayo yameonesha kuwa, katika kipindi cha kati ya miaka 1991 na 2016 kasi ya watu kuelekea kwenye dini ya Uislamu imepanda kwa asilimia 160. 

Kasi ya watu katika jamii yenye Wakristo wengi ya Australia kuelekea na kuingia kwenye Uislamu inatokana na sababu kadhaa, muhimu zaidi ikiwa ni mienendo bora na mizuri ya Waislamu na kulingana na misingi ya kiutamaduni ya nchi hiyo. Juhudi za Waislamu za kutaka kuarifisha ipasavyo misingi na nguzo za dini yao na kitabu kitakatifu cha Qur'ani ikiwa ni pamoja na kuheshimu haki za binadamu na kupambana na ubaguzi wa kijinsia na kimbari vinatajwa kuwa miongoni mwa sababu nyingine zinazowavutia zaidi watu wa jamii ya Australia hususan wenyeji asilia wa nchi hiyo katika dini ya Uislamu. Suala hilo lina umuhimu mkubwa sana katika jamii ya Australia ambayo kwa mujibu wa ripoti ya taasisi za kujitegemea za nchi hiyo, asilimia 46 ya wakazi wake asili wamekuwa wakisumbuliwa na ubaguzi wa kimbari wa aina mbalimbali katika kipindi cha miezi 6 iliyopita. 

Nukta nyingine ya kutiliwa maanani ni kuwa, ripoti iliyotolewa na Idara ya Takwimu ya Australia inaonesha kuwa, hamu ya wanawake kuelekea kwenye dini ya Uislamu nchini humo ni kubwa zaidi kuliko wanaume. Tofauti hii inatokana zaidi na itikadi za walioshiriki kwenye uchunguzi huo wa maoni wanaoamini kwamba, vazi la staha la mwanamke wa Kiislamu la hijabu lina nafasi na mchango mkubwa katika kulinda heshima na hadhi ya mwanamke katika jamii ya kiliberali ya nchi hiyo.

Wanawake wa Kiislamu nchini Australia

Wakati huo huo ripoti nyingine iliyotolewa na Taasisi ya Utafiti wa Masuala ya Asia ya Chuo Kikuu cha Melbourne inaonesha kuwa, mienendo ya Waislamu kama vile kuwaheshimu wafuasi wa dini nyingine, kupambana na ubaguzi baina ya wanadamu hususan dhidi ya wanawake na uungaji mkono wa Waislamu na kutetea kwao mazingira vimekuwa na taathira kubwa katika kuwavutia raia wengi wasio Waislamu wa Australia katika dini tukufu ya Uislamu.

Wimbi hilo kubwa na linaloongezeka la watu kuelekea kwenye Uislamu linashuhudiwa katika kipindi cha sasa licha ya njama na jitihada kubwa zinazofanywa na duru mbalimbali za Magharibi za kutaka kuufananisha au kuufungamanisha Uislamu na ugaidi na makundi yenye mienendo isiyo ya kibinadamu kama lile la Daesh.

Wapignaji wa kundi la kigaidi la Daesh

Katibu Mkuu wa Baraza la Waislamu nchini Australia, Dr Rateb Jneid ambaye amekuwa na mchango mkubwa katika kuarifisha sura halisi ya Uislamu kati ya wakazi na raia wa nchi hiyo anasema: Magaidi wamekuwa wakitumia Uislamu kama mwavuli wa kuficha uhalifu na jinai zao na kwamba Waislamu ndio wahanga wakuu wa ugaidi huo.

Ukweli ni kuwa, wimbi kubwa la watu kuelekea katika dini ya Uislamu nchini Australia licha ya propaganda chafu zinazofanywa dhidi ya dini hiyo na wafuasi wake katika nchi za Magharibi ni kielelezo cha kuongezeka uelewa na maarifa ya umma katika nchi hiyo kuhusu umuhimu na ulazima wa kutenganisha baina ya misimamo mikali katika upande mmoja na sura halisi ya Uislamu na mafundisho yake ya kibinadamu.

Mashekhe wa Kiwahabi wa Saudi Arabia wanaeneza mafundisho yasiyo sahihi kuhusu Uislamu

Hata hivyo hatupasi kusahau au kupuuza thamani ya juhudi zinazofanywa na Waislamu wa Australia katika kuhuisha kivitendo ada, desturi na mafundisho ya Uislamu kama vile kutekeleza Swala za jamaa, kufunga swaumu ya mwezi wa Ramadhani, kutangaza mafundisho ya Uislamu katika maeneo ya umma, mienendo na maadili mema ya Kiislamu katika vitendo na miamala yao na kadhalika. Haya yote yamechangia kwa njia moja au nyingine katika kuwavutia watu wa Australia katika mafundisho ya dini hiyo tukufu na kufanya mabadiliko ya kifikra katika jamii ya nchi hiyo.