Japan: Suala la kuzunguza na Korea Kaskazini limepitwa na wakati
Msemaji wa serikali ya Japan, Norio Maruyama ametaka kuzidishwa mashinikizo dhidi ya Korea Kaskazini akisema kuwa muda wa kufanya mazungumzo na nchi hiyo umepita.
Maruyama amesisitiza kuwa umefika wakati wa kuiwekea mashinikizo makubwa zaidi Pyongyang kwa ajili ya kudhibiti mienendo yake.
Kiongozi huyo wa serikali ya Japan sambamba na kuzitaka nchi zote za dunia kutekeleza vikwazo vya Umoja wa Mataifa dhidi ya Korea Kaskazini, amesema kuwa, Japan inafikiria kuiwekea vikwazo zaidi Pyongyang. Kadhalika Norio Maruyama amezitaka Russia na Uchina kutumia ushawishi wao kwa ajili ya kuhitimisha mgogoro wa eneo la Peninsula ya Korea.
Matamshi ya Msemaji wa Serikali ya Japan ya kukataa mazungumzo na Pyongyang, yametolewa baada ya serikali ya Korea Kusini kupitia Naibu Waziri wa Ulinzi wa nchi hiyo, Suh Choo-suk kutoa pendekezo kwa serikali ya Pyongyang la kufanya mazungumzo kwa ajili ya kumaliza mzozo wa mipaka wa nchi mbili, mazungumzo ambayo yanatakiwa kufanyika mwezi huu wa Julai.
Jumatatu iliyopita Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya, Federica Mogherini alitangaza kwamba, EU imeiwekea serikali ya Korea Kaskazini vikwazo vikali kwa kile alichokitaja kuwa ni hatari ya silaha za nyuklia na makombora ya nchi hiyo.