Waziri wa Ulinzi India: China na Pakistan zinajiandaa kutushambulia
Waziri wa zamani wa Ulinzi nchini India amesema kuwa, serikali ya Pakistan na China ambazo ni washindani wakubwa na hatari sana wa New Delhi, zinajiandaa kufanya shambulizi dhidi ya nchi hiyo.
Mulayam Singh Yadav ameyasema hayo akilihutubia bunge la India na kuongeza kuwa, Pakistan na China zimeungana pamoja kwa ajili ya kukabiliana na New Delhi. Sambamba na kubainisha kwamba, Pakistan pekee haiwezi kuhesabiwa kuwa hatari kwa India, amesema kuwa hivi sasa Uchina imekuwa mshindani mkuu na adui wa nchi hiyo.
Waziri huyo wa zamani wa Ulinzi nchini India ambaye anatambuliwa kwa kuwa na misimamo mikali dhidi ya China amedai kuwa, serikali ya Beijing imeficha silaha za nyuklia nchini Pakistan kwa ajili ya kupambana na nchi yake. Kadhalika Mulayam Singh Yadav amekosoa hatua ya India ya kukubali eneo la Tibet kuwa sehemu ya China na kusema kuwa, New Delhi inatakiwa iziunge mkono harakati za eneo hilo zinazopigania kujitenga. Wakati huo huo, kiongozi wa chama cha Samajwadi nchini India ametoa mwito kwa serikali ya nchi hiyo kukabiliana na kile alichosema ni upenyaji wa China katika mataifa ya Bhutan na Nepal.
Matamshi ya Mulayam Singh Yadav kuihusu China yametolewa katika hali ambayo, hivi sasa mgogoro kati ya New Delhi na Beijing kuhusu eneo la Doklam, unazidi kushika kasi siku hadi siku. Mgogoro wa kimipaka kati ya China, Bhutan na India ulianza tangu miezi kadhaa iliyopita, hasa baada ya jeshi la Uchina kuanza operesheni za ujenzi wa barabara ya mpakani katika ardhi ya Bhutan na kuingia askari wa India katika ardhi ya China. Mji wa Doklam ni kati ya maeneo ambayo serikali za Beijing na Thimphu zimekuwa zikihitilafiana kwa muda sasa.